DRC-SIASA

Upinzani nchini DRC waendelea kuvutana kuhusu uteuzi wa waziri mkuu

Baadhi ya viongozi wa baraza la maaskofu nchini DRC wanaosimamia mazungumzo ya kisiasa.
Baadhi ya viongozi wa baraza la maaskofu nchini DRC wanaosimamia mazungumzo ya kisiasa. rfi

Ni mwezi mmoja sasa tangu kutokea kifo cha aliyekuwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini DRC, Etienne Tshisekedi wa Mulumba, na bado muungano wa upinzani nchini humo unaendelea kuvutana kuhusu uteuzi wa waziri mkuu.

Matangazo ya kibiashara

Siku 10 zilizopita, maaskofu wa kanisa katoliki nchini humo ambao ndio wasuluhishi wa mzozo wa kisiasa nchini humo, waliahidi kuwa wangekuwa wametaja jina la mtu atakayechukua nafasi ya uwaziri mkuu ndani ya saa 48, ahadi ambayo hata hivyo haijaweza kutimia.

Na hata hivyo baada ya majuma kadhaa ya majadiliano, bado maridhiano hayajafikiwa.

Mwanzoni mwa wili, ugumu ulikuwa ni kupata idadi ya wagombea, sita kutoka upinzani na hatimaye kumpata mmoja kwa nafasi hiyo, hata hivyo mvutano bado uko kati ya muungano unaojiita G7 na ule wa Rassemblement ambao kila mmoja unadai una haki.

Wadadisi wa mambo hata hivyo wanaona kuwa kuna haja ya muungano wote wa upinzani kufanyiwa mabadiliko ya kimfumo ili kuruhusu kupatikana kiurahisi kwa nafasi ambayo inatakiwa.

Wakati muungano wa Rassemblement ukiwa tayari una jina la mtu wanaotaka awe waziri mkuu, rais Josephu Kabila yeye anasisitiza kupelekewa majina matatu ili kati ya hayo majina ateue mtu anayeona anafaa kuwa waziri mkuu.

Baraza la maaskofu nchini humo linaendelea na juhudi za kuwashawishi wanasiasa hao kukubaliana ili kuanza utekelezaji wa makubaliano ya Desemba 31 mwaka jana.

Umoja wa Mataifa pia umewaonya wanasiasa nchini humo kuhusu kuendelea kuvutana bila kufikia muafaka, wakisema hatua yao inasababisha kuendelea kutengeneza sintifahamu isiyo ya lazima kwa wananchi kuhusu mustakabali wa uchaguzi mkuu nchini humo.