LIBYA-WAHAMIAJI

UNICEF: Watoto wako hatarini zaidi wakijaribu kufanya safari kuingia Ulaya kutokea Libya

Baadhi ya wahamiaji watoto na vijana wakishuka kwenye mabasi katika uwanja wa ndege wa Tripoli tayari kwa kusafirishwa kurejeshwa kwenye nchi zao.
Baadhi ya wahamiaji watoto na vijana wakishuka kwenye mabasi katika uwanja wa ndege wa Tripoli tayari kwa kusafirishwa kurejeshwa kwenye nchi zao. REUTERS/Ismail Zitouny

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa idadi kubwa ya watoto bado wanahatarisha maisha yao kwa kufanya safari ya hatari kutoka nchini Libya kwenda nchini Italia.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la umoja wa Mataifa linalohusika na watoto UNICEF linasema kuwa zaidi ya watoto elfu 26, wengi wakiwa hawana wazazi wala watu wanaoambatana nao, wamevuka bahari ya Mediterania mwaka uliopita.

Kwenye ripoti yake mpya, Unicef inasema kuwa wengi wa watoto hawa wamekuwa wakifanyiwa uhalifu pamoja na udhalilishaji wa kingono wakiwa kwenye mikono ya wafanyabiashara haramu wa binadamu.

Hata hivyo Unicef inasema kuwa watoto wengi wanashindwa kutoa taarifa kuhusu vitendo walivyofanyiwa.

Unicef imeongeza kuwa pia kumekuwa na uhaba wa chakula, maji na huduma za kitabibu kwenye vituo ambavyo watoto hawa wanashikiliwa nchini Libya.

Ripoti hii inasema kuwa watoto wengi ambao hawasindikizwi na wazazi wap, wamekuwa wazoefu wa mazingira ya wahamiaji katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Ripoti hii iliyopewa jina la "Safari ya hatari kwa watoto" imeanisha hatari ambazo watoto hawa wamekuwa wakikabiliwa nazo kabla, wakati na hata baada ya kufanya safari yao kuelekea Italia.