DJIBOUTI-UFARANSA

Nini kipo nyuma ya pazia kwenye ziara ya rais wa Djibouti nchini Ufaransa

Rais wa Ufaransa, François Hollande akisalimiana na rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh kwenye Ikulu l'Elysée. Tarehe 28 Februari 2017.
Rais wa Ufaransa, François Hollande akisalimiana na rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh kwenye Ikulu l'Elysée. Tarehe 28 Februari 2017. REUTERS/Philippe Wojazer

Rais wa Djibouti yuko ziarani jijini Paris, Ufaransa, ambapo amekutana na mwenyeji wake rais Francois Hollande, Jumanne ya wiki hii, ambapo wamebadilishana mawazo kuhusu usalama wa ukanda, vita dhidi ya ugaidi, msaada wa kimaendeleo na ushirikiano wa nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa "Francophonie".

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo ziara ya rais, Ismaïl Omar Guelleh, ina maswali mengi ambapo wachambuzi wa mambo wanahoji ni urafiki wa aina gani uliopo kati ya nchi hizi mbili?

Akiwa amebakiza wiki chache tu kabla ya kuondoka madarakani, rais Hollande amekutana na rais wa Djibouti kwenye ikulu ya Paris, ziara ambayo kwa sehemu kubwa imekuwa ya siri na hakuna mengi yaliyowekwa wazi kuhusu mazungumzo yao.

Licha ya kuwa rais Ismaïl Omar Guelleh, amejaribu kueleza ni kwanini alichelewa kufanya ziara nchini humo, wadadisi wa mambo wanasema kuna hali tete ya uhusiano baina ya nchi hizi mbili na ziara yake ililenga kuondoa sintofahamu hiyo.

Kulikuwa na mzozo katika uchaguzi wa mwaka jana nchini Djibouti, ambapo Ufaransa ilimuondoa balozi wake nchini humo kupinga kilichofanywa na tume ya uchaguzi pamoja na vifo vya mwaka 2015 mjini Buldocqo.

Rais wa Ufaransa, François Hollande akiwa na mgeni wake rais wa Djibouti, Ismaïl Omar Guelleh, kwenye Ikulu ya l'Elysée. 28 Februari 2017.
Rais wa Ufaransa, François Hollande akiwa na mgeni wake rais wa Djibouti, Ismaïl Omar Guelleh, kwenye Ikulu ya l'Elysée. 28 Februari 2017. REUTERS/Philippe Wojazer

Ufaransa bado imeendelea kusalia msiri kuhusu uhusiano iliyonao na Djibouti ambapo Marekani ambayo ina ubalozi pia nchini humo, ilishasema wazi kuwa inataka kwanza kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa kwenye magereza mbalimbali nchini humo.

Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa Ufaransa na Marekani licha ya kutoridhishwa na namna nchi hiyo inavyoendeshwa, hawawezi kuitenga moja kwa moja kwa kuwa ni mshirika mkubwa katika vita dhidi ya uharamia baraharini na ugaidi.

Djibouti ndio nchi yenye idadi kubwa ya wanajeshi wa Ufaransa, vikosi ambavyo vimekuwa vikitumia pwani ya nchi hiyo kurusha ndege zake za kivita kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati, Yemen, Iraq na Mali.

Djibouti pia ndio njia kuu inayounganisha mataifa ya nchi za mashariki ya kati na pia moja kati ya nchi zenye bandari nzuri.

Nchi ya China imefanya uwekezaji mkubwa kwenye nchi ya Djibouti hasa ukizingatia kuwa, imeendelea na uwekezaji mwingi kwenye nchi za Afrika na hasa katika miundo mbinu.

Shirika la fedha duniani IMF, linatabiri kuwa uchumi wa Djibouti utakuwa kwa asilimia 7 licha ya changamoto zinazoikabili nchi hiyo.