DRC-MONUSCO

UN: Vyombo vya usalama DRC vilitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji

Muandamanaji wa DRC akiwa kwenye pikipiki akikabiliana na polisi wa kutuliza ghasia.
Muandamanaji wa DRC akiwa kwenye pikipiki akikabiliana na polisi wa kutuliza ghasia. REUTERS/Robert Carrubba

Umoja wa Mataifa umevituhumu vyombo vya ulinzi na usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, kuwa vilitumia nguvu kubwa kupita kiasi mwezi Desemba mwaka jana, wakati walipokabiliana na waandamanaji waliokuwa wanapinga rais Joseph Kabila kusalia madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Kati ya Desemba 15 na 31 mwaka 2016, watu wanaokadiriwa kufikia 40 waliuawa na wengine zaidi ya 147 walijeruhiwa kwenye miji mbalimbali nchini DRC, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa na ile ya DRC (BCNUDH).

Waaandamanaji walikuwa wanapinga rais Kabila kuendelea kusalia madarakani hata baada ya muhula wake kutamatika Desemba 20 mwaka jana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wengi walioathirika walikuwa ni raia wasio na silaha ambapo walilengwa kwa risasi kwenye maeneo ya juu ya mwili baada ya vyombo vya dola kutumia risasi za moto na hasa jeshi la nchi hiyo, wakiwemo walinzi wa rais na polisi wa jeshi ambao mara nyingi huwa hawapewi mafunzo ya kudhibiti maandamano.

Ripoti imeongeza kuwa wakati huohuo watu zaidi ya 917 walikamatwa na vyombo vya usalama nchi nzima.

Tume hiyo inasema wengi ya waliokamatwa inaamini walikamatwa wakati wakifanya maandamano ya amani na walikuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba kuandamana kwa amani.

Kamati ya uchunguzi imesema kuwa "Kukosekana kwa ushirikiano kati ya vyombo vya dola vya nchi hiyo, kutopewa nafasi kutembelea vituo vya kijeshi walikohifadhiwa waandamanaji, idara ya usalama wa taifa, hospitali na vyumba vya kuhifadhia maiti, ambako inaaminika vitendo vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu vilitekelezwa, kumetia dosari uchunguzi wao.

Waziri wa haki za binadamu nchini DRC, Marie-Ange Mushobekwa, ameeleza kwenye ripoti yake kuwa, waangalizi wao walinyimwa nafasi ya kutemebelea vituo vya kijeshi vinavyowahifadhi watu waliokamatwa, kwa kile alichosema ni sababu za usalama wa taifa na ulinzi.

Hii si mara ya kwanza kwa vyombo vya dola nchini DRC kutuhumiwa kutumia nguvu kubwa dhidi ya maandamano ya amani nchini humo, ambapo jumuiya ya kimataifa imeendelea kukashifu vitendo hivyo huku hatua dhidi ya wahusika zikishindwa kuchukuliwa.