MISRI

Mahakama ya juu Misri yamkuta hana hatia ya mauaji Hosni Mubarak

Rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak akiwa mahakamani kwenye moja ya kesi zake.
Rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak akiwa mahakamani kwenye moja ya kesi zake. REUTERS/Stringer/Files

Mahakama ya juu nchini Misri imemkuta hana hatia ya mauaji ya waandamanaji aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Hosni Mubarak, uamuzi huu ni wa mwisho na huenda ukashuhudia kiongozi huyo akiachiwa huru.

Matangazo ya kibiashara

Mubarak alikuwa amehukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 2012 lakini mahakama ya rufaa iliagiza kesi yake kusikilizwa upya, mahakama ambayo miaka miwili baadae imeyafuta mashtaka dhidi yake.

Kwa mujibu wa sheria za Misri, uamuzi wa mahakama ya juu, huwa ni uamuzi wa mwisho usiokatiwa rufaa.

Kesi hii ilikuwa ni kesi yake ya mwisho, baada ya waendesha mashtaka kumfungulia mashtaka lukuki dhidi yake punde tu baada ya kujiuzulu mwaka 2011.

Alituhumiwa kwa kuchochea mauaji dhidi ya waandamanaji wakati wa maandamano ya siku 18, ambapo watu zaidi ya 859 waliuawa wakati polisi walipoingia kati kuwasambaratisha waandamanaji.

Mubarak, mwenye umri wa miaka 88 hivi sasa, ametumia muda mwingi akiwa kwenye hospitali moja ya kijeshi toka alipokamatwa mwaka 2011.

Mwezi Januari mwaka 2016, mahakama ya rufaa ilithibitisha hukumu yake ya awali ya kifungo cha miaka mitatu jela yeye pamoja na watoto wake wawili kwa tuhuma za rushwa.

Hata hivyo uamuzi ule ulizingatia muda ambao walitumia gerezani toka walipokamatwa, watoto wake wote wawili Alaa na Gamal waliachiwa.