Serikali ya DRC yafutilia mbali ripoti ya Umoja wa Mataifa
Imechapishwa:
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imejibu baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa kutuhumu polisi kuwaua waandamanji kwa makusudi mjini Kinshasa.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imefutilia mbali ripoti hiyo na kusema kwa ni mambo yaliyopangwa kwa kuchafua viongozi wa DR Congo
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 40 waliuawa katika matukio haya wakati ambapo serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imebaini kwamba watu 31 pekee ndio waliouawa.
"Serikali inabaini kwamba hakuna ukweli wowote kattika ripoti hiyo, ni mambo yaliyotengenezwa kwa kuweza kuchafua viongozi wa DR Congo," amesema Lambert Mende, msemaji wa serikali ya DR Congo.
Katika maoni yake, "lengo la ripoti hiyo ilikua kudhoofisha mahakama, taasisi za kisiasa na kiusalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na si kwa waathirika kutendewa haki."
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, iliyotolewa Jumanne, inaeleza ukiukwaji unaodaiwa kufanywa na vikosi vya usalama kwa waandamanji walioandamana dhidi ya Kabila mwezi Desemba 2016.
Katika ripoti ya Umoja wa Mataifa, imeelezwa kuwa baadhi ya waandamanaji waliuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la polisi.
Upinzani unapinga Joseph Kabila kuendelea kusalia madarakani wakati ambapo muhula wake wa pili ungelimalizika tarehe 19 Desemba 2016.