MSUMBIJI

Msumbiji: Kiongozi wa Renamo Afonso Dhlakama atangaza muda zaidi wa kusitisha mapigano

Kiongozi wa chama cha Renamo nchini Msumbiji, Afonso Dhlakama, hapa ilikuwa mwaka 2013 alipozungumza na wanahabari kwenye milima ya Gorogonsa.
Kiongozi wa chama cha Renamo nchini Msumbiji, Afonso Dhlakama, hapa ilikuwa mwaka 2013 alipozungumza na wanahabari kwenye milima ya Gorogonsa. AFP PHOTO / JINTY JACKSON

Kiongozi wa upinzani nchini Msumbiji, Afonso Dhlakama, Ijumaa ya Machi 3, ametangaza kuongeza muda wa miezi miwili ziaid ya usitishaji wa mapigano kati ya vikosi vyake vya Renamo na vile vya Serikali.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na kutangaza nyongeza ya muda huo, kiongozi huyo pia ametangaza kuwa watashiriki mazungumzo mapya Jumatatu ya wiki ijayo, Machi 6 mwaka huu.

Dhlakama amesema kuwa, wataongeza muda wa siku 60 ili kuruhusu sio tu muda wa mazungumzo lakini pia kuzuia vifo zaidi.

Akizungumza na wanahabari kwa njia ya simu kutokea kwenye milima ya Gorongosa, ambako amekimbilia toka mwezi October 2015, kiongozi huyu wa Renamo amesema anaongeza muda hadi April 4 mwaka huu.

Licha ya matukio kadhaa ya uvunjifu wa makubaliano ya kusitisha mapigano, Dhlakama bado anaona kuwa kwa sehemu kubwa makubaliano hayo yameheshimiwa na anatamani yaendelee kuheshimiwa ili kutozuia kufanyika kwa mazungumzo zaidi.

Dhlakama amekiri kuwa mapigano yanayoendelea nchini humo na mvutano wa kisiasa unaoshuhudiwa, vimesababisha uchumi wa taifa hilo kutetereka.

Mwezi Februari mwaka huu, rais wa Msumbiji Filipe Nyusi alitangaza kuanza kwa raundi ya mazungumzo mapya bila ya kuwa na usimamizi wa waangalizi wa kimataifa, ambao kwa muda sasa wamekuwa wakiratibu mazungumzo hayo.

Dhlakama amesema kuwa "wakati wapatanishi walipoondoka, watu wa Msumbiji na waangalizi wa kisiasa walianza kuwa na sintofahamu na kufikiri kuwa mazungumzo yameanguka," alisema kiongozi huyo.

Renamo inasema imefikia muafaka na upande wa Serikali kuhusu kufanyika kwa mazungumzo mapya, ambapo imeongeza kuwa haikuwa kazi rahisi kuratibu mchakato wa kufanyika kwa mazungumzo mengine.