DRC-USALAMA

Operesheni ya kuwatafuta raia waliotekwa nyara yaaendelea Maniema

Mgodi wa Namoya katika Jimbo la Maniema, mashariki mwa DRC.
Mgodi wa Namoya katika Jimbo la Maniema, mashariki mwa DRC. Banro

Maafisa wa usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaendelea na msako kuwatafuta raia wa kigeni waliotekwa nyara Alhamisi wiki hii katika mkoa wa Maniema Mashariki mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Watu waliotekwa ni wafanyikazi katika mgodi wa dhahabu Banro Corporation ulioko Namoya, mmoja raia wa Tanzania, Ufaransa na watatu kutoka DRC.

Ripoti zinasema kuwa watekaji nyara ambao ni waasi wanataka kiasi kikubwa cha fedha lakini pia kupewa mkataba wa ahadi ya kutengenezewa barabara na kuendeleza miundo mbinu mingine ya kijamii kwenye eneo hilo.

Wapiganaji kutoka kundi la Raia Mutomboki waliwateka raia hao na kukimbia nao msituni huku wakiwatishia kuwaua raia wengine waliojaribu kuwazuia kutekeleza utekaji huo, ameongeza afisa wa eneo hilo Balthazar Hemedi Kabemba.

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imesema tayari imeanza mawasiliano na maofisa wa mgodi huo kupata taarifa ya kile kilichotokea.

Mwezi uliopita polisi watatu na moiganaji mmoja walikufa wakati yalipotokea makabiliano na majambazi waliojaribu kuvamia mgodi mwingine wa Twangiza.