SUDAN-UN

Amnesty International: Ni aibu kwa UN kutochunguza matumizi ya silaha za kemikali Darfur

Rais wa Sudan, Omar el-Beshir wakati alipotembelea eneo la Darfur
Rais wa Sudan, Omar el-Beshir wakati alipotembelea eneo la Darfur Reuters

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, juma hili limeukumbusha umoja wa Mataifa kuhusu uchunguzi wa tuhuma za matumizi ya silaha za kemikali yaliyofanywa na vikosi vya Serikali ya Sudan kwenye jimbo la Darfur, Amnesty ikisema itakuwa ni aibu ikiwa suala hilo halitachunguzwa.

Matangazo ya kibiashara

Amnesty ilisema kwenye taarifa yake ya mwezi Septemba mwaka jana kuwa, inao ushahidi usio na shaka kuwa vikosi vya Serikali mara kadhaa vilitumia silaha za kemikali kwenye milima ya jimbo la Darfur kati ya mwezi Januari na Agosti mwaka 2016 ambapo watu kati ya 200 na 250 waliuawa, wakiwemo watoto.

Ofisi ya umoja wa Mataifa inayohusika na kupiga vita matumizi ya silaha za kemikali OPCW, ilisema wakati ule kuwa, ilihitaji taarifa zaidi na ushahidi ili kufikia hitimisho kwa kutumia ushahidi wa Amnesty International.

Amnesty imefufua suala hili ikitaka kufanyike uchunguzi huru na kamili wa OPCW, wito unaokuja wakati ambapo juma hili ofisi hiyo ya umoja wa Mataifa itakuwa na mkutano wa siku nne mjini The Hague.

"Kushindwa kwa nchi wanachama wa OPCW kuanzisha uchunguzi itakuwa ni ishara na jambo la aibu katika kutumiza wajibu wake," amesema Michelle Kagari kutoka shirika la Amnesty.

Amnesty inasema kuwa baadhi ya nchi wanachama wa OPCW walionesha kusikitishwa na kukemea matumizi haya ya silaha za kemikali, lakini maneno tu hayatoshi bila kuchukua hatua.

"Lazima wahakikishe hatua muhimu zinachukuliwa kubaini asili ya shambulio lenyewe na ni kwa kiasi gani Serikali ya Khartoum inazo silaha za kemikali na kuishinikiza Sudan kushirikiana na OPCW".

Amnesty imeongeza kuwa nchi wanachama wa OPCW zinatakiwa pia ziagize kupewa ushirikiano wa uchunguzi kwenye mkoa wa Jebel Marra jimboni Darfur ambako shambulio hili linadaiwa kutekelezwa.