DRC

Familia ya Tshisekedi ya ahirisha kurejesha mwili wake mwishoni mwa juma hili

Jeneza lenye mwili wa Etienne Tshisekedi wakati alipoagwa na wafuasi wake jijini Brussels. Tarehe 5 Januari 2017
Jeneza lenye mwili wa Etienne Tshisekedi wakati alipoagwa na wafuasi wake jijini Brussels. Tarehe 5 Januari 2017 REUTERS/Francois Lenoir

Mwili wa aliyekuwa kinara wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Etienne Tshisekedi wa Mulumba, hautarejeshwa nchini humo Jumamosi ya wiki hii kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali, familia yake imesema.

Matangazo ya kibiashara

Kaka wa maerehemu, Gerard Mulumba, ambaye kaka yake alifariki Februari Mosi mwaka huu akipatiwa matibabu jijini Brussels Ubelgiji, amesema kuwa raia wengi mjini Kinshasa wanapinga kiongozi wao kwenda kuzikwa kwenye makaburi ya katikati ya mji, hali iliyowafanya familia kubadili mawazo.

Hatua hii imekuja kwa kushtua kwakuwa familia ya Tshisekedi yenyewe ilikuwa imetangaza tarehe 11 Machi ya mwezi huu, kuwa mwili wa kiongozi huyo ungerejeshwa jijini Kinshasa kwa mazishi.

Mulumba amesema kuwa, eneo la Gombe lililokuwa limekubaliwa awali kati yao na Serikali, limeonekana kutowavutia maelfu ya wafuasi wa Tshisekedi pamoja na makundi mengine ambayo yanamuunga mkono.

Katika hatua nyingine, msemaji wa Serikali ya DRC, Lambert Mende, amesema Serikali haina uwezo wa kuingilia uamuzi huu kwakuwa unabaki kuwa wa familia.

Mende ameongeza kuwa uamuzi wa ni wapi mwili wa Tshisekedi utahifadhiwa, yanabaki kuwa maamuzi ya Gavana wa jimbo.

Hata hivyo bado wafuasi wengi wa Tshisekedi bado wanapinga kurejeshwa kwa mwili wake huku makubaliano ya Desemba 31 mwaka jana yakiwa bado hayajatekelezwa, wengi wanataka kwanza makubaliano hayo yaanze kutekelezwa kabla ya mwili wake kurejeshwa.

Wapo pia wanaotaka kiongozi huyo kuzikwa kwa heshima zote na kuwekwa kwenye makaburi ya mashujaa jijini Kinshasa kama sehemu ya kuonesha mchango wake wakati wa uhai wake katika kupigania Demokrasia.