SOMALIA-UN

Katibu mkuu wa UN atoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuisaidia Somalia

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akizungumza mjini Mogadishu baada ya kukutana na rais wa Somalia, Farmajo. Tarehe 7 Machi 2017.
Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akizungumza mjini Mogadishu baada ya kukutana na rais wa Somalia, Farmajo. Tarehe 7 Machi 2017. REUTERS/Feisal Omar

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Antonio Guterres, juma hili ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua ili kudhibiti baa la njaa nchini Somalia, ambako madhara yake yamewaacha watu zaidi ya milioni tatu wakiwa hawana chakula.

Matangazo ya kibiashara

Nchi ya Somalia inakabiliwa na baa la njaa kwa mara ya tatu katika kipindi cha miaka 25, huku vita vya muda mrefu na ugombanianaji wa madaraka vikiwa sehemu ya sababu ya kinachoshuhudiwa sasa.

Mwaka 2011 njaa ilisababisha vifo vya watu laki mbili na elfu sitini kwenye pembe hiyo ya Afrika.

"Kuna nafasi ya kuzuia madhara zaidi, lakini tunahitaji msaada mkubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ili kuzuia kujirudia kwa madhara yaliyoshuhudiwa mwaka 2011," amesema Guterres.

Katibu mkuu Guterres aliwasili mjini Mogadishu Somalia Jumanne ya Machi 7 kwa ziara fupi ambayo itashuhudia ikimpeleka hadi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani wa nchi hiyo iliyoko kaskazini mwa nchi.

Guterres amekutana na rais Mohamed Abdullahi Mohamed, kiongozi maarufu ambaye hivi karibuni alishinda uchaguzi wa nchi hiyo na kuibua matumaini mapya ya kuimarisha na kudumisha usalama wa nchi hiyo.

"Sababu ya Guterres kuja leo nchini kunaonesha uungaji mkono wake kwa wananchi wa Somalia hasa wakati huu tukikabiliwa na janga la kibinadamu," amesema rais Abdullahi ambaye ni maarufu kwa jina la Farmajo.

"Tuna ukame ambao matokeo yake utasababisha njaa kali ikiwa hatutapokea msaada ndani ya miezi miwili ijayo," amesema rais Farmajo.

Wakati Somalia ikielekea kurejea kuwa tulivu, rais Farmajo ameonya baada ya kushinda kiti hicho kuwa, hakutakuwa na suluhu ya haraka kwa nchi hiyo.

"Matatizo yenu yalitengenezwa katika kipindi cha miaka 20 ya vita na njaa, suluhu itahitaji miaka 20 zaidi," amesema rais Farmajo wakati alipozungumza mjini Mogadishu mwezi uliopita.

Somalia ni miongoni mwa mataifa matatu duniani yanayokabiliwa na njaa mbaya, ambapo zimo pia nchi za Yemen na Nigeria huku nchi ya Sudan Kusini yenyewe tayari imetangaza baa la njaa.