MALEMA-AFRIKA KUSINI

Mahakama yamzuia Malema kutoa matamshi ya uchochezi kuhusu ardhi

Julius Malema, kiongozi wa chama cha EFF nchini Afrika Kusini.
Julius Malema, kiongozi wa chama cha EFF nchini Afrika Kusini. REUTERS/Siphiwe Sibeko

Mahakama nchini Afrika Kusini imetoa amri kumzuia kiongozi wa chama cha upinzani nchini humo cha EFF, Julius Malema, kuwataka wafuasi wake kuchukua ardhi kwa nguvu, wakati huu akikabiliwa na mashtaka mawili ya kuitisha raia kuchukua ardhi kwa nguvu.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama mjini Pretoria, imesema kuwa Malema kinara wa chama cha The Economic Freedom Fighter, atakamatwa ikiwa atakutwa na hatia ya kukaidi amri hiyo ya mahakama.

Uamuzi huu wa mahakama umetokana na kesi iliyowasilishwa na watu wa jamii ya Afrikaner, AfriForum, ambao walieleza kuguswa na matamshi ya Malema aliyetaka raia kuwanyang'anya ardhi kwa nguvu wazungu.

Hata hivyo Julius Malema mwenyewe hakuwepo mahakamani wakati hukumu hiyo ikitolewa.

Malema anakabiliwa na mashtaka mawili yanayohusiana na wito wake wa kuwaambia watu weusi wachukua ardhi kwa nguvu kutoka kwa wazungu nchini humo.

Mwezi Novemba mwaka 2016, katika moja ya kesi inayomkabili, alirejelea matamshi yake ya kuwataka wananchi weusi wachukua ardhi yao akiituhumu Serikali kw akushindwa kuigawa ardhi hiyo kwa zaidi ya miaka 22 toka kuanguka kwa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.

"Umeipenda, ichukue, ni mali yako..ni ardhi iliyochukuliwa kutoka kwetu na wazungu kwa nguvu kupitia mauaji ya halaiki," Malema aliwaambia wafuasi wake.

Malema alisema kamwe hatishwi na amri ya mahakama kuhusu kwenda jela.

Julius Malema, ambaye alifukuzwa ndani ya chama cha ANC mwaka 2012 anatarajiwa kurejea mahakamani hapo May 5 mwaka huu.

Kiongozi huyu anakabiliwa na mashtaka mengine kama haya, matamshi ambayo aliyatoa mwaka 2014.

Chama cha EFF ambacho kilishinda kwa asilimia 6 kwenye uchaguzi mkuu wa rais mwaka 2014, kimekuwa kikihubiri kuhusu unyang'anyi wa ardhi kutoka kwa watu weusi kulikofanywa na watu weupe.

Wiki iliyopita kamati kuu ya chama tawala cha ANC, ilipiga kura kupinga mapendekezo ya sheria ya umiliki ardhi.