DRC-UN-MAUAJI

Makaburi ya halaiki DRC: Lambert Mende akosoa UN

Wakaazi wa mji wa Kasai wakikimbia, baada ya risasi kusikika karibu na kambi ya kijeshi.
Wakaazi wa mji wa Kasai wakikimbia, baada ya risasi kusikika karibu na kambi ya kijeshi. HCR/Celine Schmitt

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lambert Mende amelaani msimamo wa Kamishna Mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, na kubainisha kuwa uchunguzi wa mahakama ya DR Congo unaendelea.

Matangazo ya kibiashara

"Majaji wetu wamegundua zaidi ya makaburi 3 ya halaiki na makosa makubwa ya Kamuina Nsapu" Lambert Mende ameiambia RFI Jumatano wiki hii. Waziri huyo wa Mawasiliano wa DR Congo amesema kuwa makaburi hayo ya halaiki yalichimbwa na wanamgambo wa kiongozi wa kiroho wa kundi la Bundu Dia Kongo (BDK), Kamuina Nsapu, ambao walikua wakiwazika watu baada ya kuwaua.

Lambert Mende ameongeza kuwa watu hao walikua wakiuawa katika mazingira mabaya yenye kutatanisha. Viongozi wa kimila, wasomi na polisi ni miongoni mwa watu waliouawa na kundi hilo, amesema Lambert Mende.

Hivi karibuni Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, ilitaka kufanyike uchunguzi wa kina kuhusu vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyofanywa dhidi ya raia wa kawaida kwenye maeneo yenye vurugu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya kugundulika kwa kaburi la pamoja.

Mkuu wa tume hiyo, Zeid Ra'ad Al Hussein, aliipongeza serikali ya DRC kwa kuchukua hatua za haraka kuchunguza mauaji na matukio mengine makubwa ya unyanyasaji na ukatili uliofanywa kwenye jimbo la Kasai na Lomani, lakini akasema uchunguzi wa Umoja wa Mataifa unahitajika pia.

Mwezi Februari mwaka huu, video ya dakika 7 iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, ambayo ilionekana imerekodiwa kwa simu ya kiganjani, ikionesha mauaji ya watu wasio na silaha wanawake na wanaume waliouawa na wanajeshi  kwenye eneo linalodhaniwa kuwa ni Kasai.