ICC-AFRIKA KUSINI

Serikali ya Afrika Kusini yabadili uamuzi wa kujitoa kwenye mahakama ya ICC

Jengo la mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC.
Jengo la mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC. REUTERS/Jerry Lampen/File Photo

Nchi ya Afrika Kusini imetangaza rasmi kubadilisha uamuzi wake wa awali kuhusu kujitoa kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC, hatua inayokuja baada ya uamuzi wa mahakama mwezi uliopita kuagiza Serikali kuondoa hati ya kujitoa na kwamba ingekuwa kinyume cha katiba.

Matangazo ya kibiashara

Notisi ya nchi ya Afrika Kusini kuondoa azma yake ya kujitoa kwenye mahakama ya ICC, iliwekwa kwenye tovuti ya mahakama ya ICC, licha ya kuwa Serikali ya Pretoria haikuweka wazi ikiwa ndio nia yake ya kujitoa bado itasalia.

Nchi ya Afrika Kusini ilifanya uamuzi wa kuanza kujiondoa kwenye mahakama ya ICC mwezi Octoba mwaka jana, baada ya kukosolewa kwa kushindwa kumkamata rais wa Sudan, Omary Bashir.

Mahakama ya ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa rais Bashir anayetuhumiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita, lakini mamlaka nchini Afrika Kusini zilikataa kumkamata ikisema alikuwa analindwa kwa mujibu wa sheria.

Uamuzi wa nchi hiyo kujitoa kwenye mahakama ya ICC uliibua ukosolewaji mkubwa, lakini Jumanne ya tarehe 7, Serikali ilimtaarifu katibu mkuu Antonio Guterres, kumueleza kuwa mchakato waliokuwa wameuanza ulikuwa kinyume cha katiba.

Taarifa ya Serikali inasema kuwa "ili kuheshimu uamuzi wa mahakama kuu, natangaza kuondoa hati ya kuanza mchakato wa nchi kujitoa kwenye mkataba wa Roma," ilisema taarifa hiyo kwa katibu mkuu.

Mwezi uliopita mahakama kuu ya mjini Gauteng, iliiagiza Serikali kuondoa mara moja hati ya nchi hiyo kujitoa kwenye mahakama ya ICC na kwamba ilikuwa kinyume cha katiba na bunge halikuulizwa.

Kesi hiyo iliwasilishwa na chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance.