AFRIKA KUSINI

ICC yaitaka Serikali ya Afrika Kusini kufika mahakamani hapo April 7

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Reuters/Rogan Ward

Mamlaka nchini Afrika Kusini wametakiwa kutokea mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC iliyoko mjini The Hague Uholanzi, Aprili 7 mwaka huu kuhusiana na kushindwa kwao kumkamata rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, wakati alipofanya ziara miaka miwili iliyopita.

Matangazo ya kibiashara

Ayesha Johaar, mshauri masuala ya sheria wa Serikali, amesema kuwa utawala wa Pretoria umetakiwa kuhudhuria kikao cha mahakama hiyo kwa kushindwa kumkamata rais Bashir wakati walikuwa wanajua kabisa kuna hati ya kukamatwa ilikuwa imetolewa dhidi yake.

"Hati iliyotolewa na ICC inahusu kupewa maelezo ya kwanini Serikali ilishindwa kutumiza masharti ya mkataba wa Roma kama mwanachama kumkamata rais wa Sudan," alisema mshauri.

Serikali ya Pretoria ilikuwa imetangaza nia yake ya kujiondoa kwenye mahakama ya ICC mwaka 2015, baada ya nchi hiyo kukosolewa kwa kushindwa kumkamata Bashir, ambaye anatuhumiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita aliyoyatekeleza kwenye jimbo la Darfur.

Mahakama kuu nchini Afrika Kusini, mwezi uliopita ilizuia mchakato wa Serikali kutaka kujiondoa kwenye mahakama hiyo.

Hata hivyo mwanasheria mkuu wa Serikali Michael Masutha amesisitiza kuwa Serikali itaendelea mbele na mchakato wake wa kujiondoa kwenye mahakama hiyo, kwakuwa uamuzi wa mahakama kuu ulijikita katika Serikali kufuata taratibu kujitoa.

Na kwa kutii uamuzi wa mahakama kuu, Serikali tayari imetangaza kuondoa hati yake kwenye umoja wa Mataifa kuhusu kujiondoa kwenye mahakama ya ICC.