SUDAN KUSINI

Juba yatangaza ada mpya za kupata kibali cha kazi kwa wafanyakazi wa kigeni, mashirika ya misaada ya kosoa

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir.
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir. REUTERS/Jok Solomon

Licha ya kukabiliwa na vita pamoja na baa la njaa na kuhitaji msaada, Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuongeza ada ya kupata kibali cha kufanyia kazi nchini nchini humo, kutoka Fold 100 za Sudan hadi kufikia dola elfu 1 za Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Taifa hili changa zaidi duniani limekuwa likikabiliwa na vita toka mwaka 2013, wakati rais Salva Kiir alipomfuta kazi makamu wake Riek Machar, hali iliyosababisha kuzusha mapigano na mgawanyiko wa kikabila nchini humo.

Mwezi uliopita, umoja wa Mataifa ulitangaza baa la njaa kwenye baadhi ya maeneo nchi hiyo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa hatua hii kuchukuliwa katika kipindi cha miaka sita.

Watu karibu nusu milioni, wanaelezwa kuwa watakosa huduma muhimu ikiwemo chakula.

Licha ya kukabiliwa na hali mbaya, utawala wa Juba sasa utatoza kiasi cha dola elfu 10 kwa wageni wanaofanya kazi rasmi, dola elfu 2 kwa wale wanaofanya kazi za kawaida na dola elfu 1 kwa kazi nyingine kuanzia Machi mosi mwaka huu.

Edmund Yakani, mkurugenzi mtendaji wa shirika moja la misaada nchini humo, amesema kuwa tangazo hili la Serikali linalenga kupunguza idadi ya wafanyakazi wa misaada.

"Ukweli ni kwamba gharama hizi za kupata kibali ni kubwa sana kwa wafanyakazi wa misaada, hasa ukizingatia kuwa asilimia 90 ya wafanyakazi wa kigeni wanaotaka kufanya kazi Sudan Kusini ni wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu," alisema mkurugenzi huyo.