MALI

Kundi jipya la Kijihadi nchini Mali lakiri kuhusika na shambulio lililoua wanajeshi 11 wiki iliyopita

Askari wa Mali wakitazama moja ya matukio ya kujitoa muhanga yaliyotekelezwa na makundi ya kijihadi kwenye mji wa Gao.
Askari wa Mali wakitazama moja ya matukio ya kujitoa muhanga yaliyotekelezwa na makundi ya kijihadi kwenye mji wa Gao. REUTERS/via Reuters TV TPX IMAGES OF THE DAY

Kundi linalounga mkono dini ya Kiislamu na Waislamu, kundi jipya ambalo limeundwa baada ya makundi mengine ya kijihadi kuungana kutoka ukanda wa Sahel, limekiri kuhusika kwenye shambulio la kwenye kambi moja ya kijeshi, ambapo wanajeshi 11 wa Mali waliuawa.

Matangazo ya kibiashara

Shambulizi la kwenye kambi ya jeshi ya Boulikessi katikati mwa nchi ya Mali, jirani kabisa na mpaka na Burkina Faso, shambulio lililotekelezwa Machi 5 mwaka huu, limetekelezwa na kundi hilo ambalo limekiri kupitia mtandao wake.

Kundi la SGIM ambalo linaundwa na makundi mengine kama ya Iyad Ag na lile la Algeria Mokhtar Belmoktar, juma lililopita walitangaza kuunda katiba yao.

Kwenye taarifa yake, kundi hilo linadai liliwaua mamia ya askari wa Mali, kuharibu magari na kupora mamia ya silaha, huku likidai kuwa ni wapiganaji wake wawili tu ndio waliopoteza maisha kwenye shambulio hilo.

Uundwaji wa kundi la "Support Group for Islam and Muslims" liliwekwa hadharani kupitia mkanda wa video, uliomuonesha kiongozi wa kundi hili jipya akiwa sambamba na viongozi wa makundi mengine yaliyoungana.

Makundi yote haya yaliyoungana, yanahusishwa kuwa na uhusiano wa karibu na mtandao wa kigaidi duniani wa Al-Qaeda, makundi ambayo yalifanikiwa kuchukua eneo la kaskazini mwa Mali March na Aprili 2012.

Hata hivyo makundi haya yalifurushwa kutoka kaskazini mwa Mali baada ya kutekelezwa kwa operesheni kubwa iliyohusisha vikosi vya kimataifa, operesheni iliyoanzishwa mwaka 2013 baada ya kuanzishwa na nchi ya Ufaransa, operesheni ambayo inaendelea.