DRC-UNSC

Katibu mkuu wa UN aagiza kupelekwa kwa polisi 320 nchini DRC

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Antonio Guterres
Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Antonio Guterres REUTERS/Feisal Omar

Katibu Mkuu wa Umoja Antonio Guterres jana Ijumaa amelitaka Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa kupeleka polisi wa ziada wapatao 320 wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya mpango wa kukomesha mzozo kuhusu uchaguzi kukwama na kusababisha hofu ya vurugu mpya.

Matangazo ya kibiashara

Katika ripoti iliyopatikana na shirika la habari la Ufaransa AFP, Guterres amesema anasikitishwa sana na kuongezeka kwa kasi kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na kusema kwamba vikosi vipya vya polisi kwa ajili ya ujumbe wa MONUSCO vitasaidia kulinda raia.

Vikosi viwili vya ziada vitapelekwa katika mji wa pili kwa ukubwa wa Lubumbashi na Kananga nchini DRC, miji ambayo inaweza kuwa maeneo yenye joto kali la uchaguzi na kule ambako hakuna polisi wa Umoja wa Mataifa.

Guterres amesema uingiliaji huo wa haraka katika maeneo hayo muhimu ya mijini utaongeza uwezo wa ujumbe huo kulinda raia, pamoja na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na majengo, ikiwa kutazuka vurugu zinazohusiana na uchaguzi.

Umoja wa Mataifa una karibu wanajeshi elfu 19 nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, idadi ambayo ni kubwa zaidi na wenye gharama kubwa kwa ujumbe wake wa kulinda amani.