AFRIKA KUSINI-NIGERIA-USHIRIKIANO

Afrika Kusini na Nigeria kuungana dhidi ya ubaguzi wa wageni

Raia wa kigeni wakijihami kwa mawe na marungu kwa kujilinda katika mitaa ya Pretoria (picha ya zamani).
Raia wa kigeni wakijihami kwa mawe na marungu kwa kujilinda katika mitaa ya Pretoria (picha ya zamani). Getty Images

Wakati wa vurugu zikiendelea, maduka mengi na nyumba zinazomilikiwa na raia wa kigeni nchini Afrika Kusini zilishambuliwa katika vitongoji vya watu duni vya miji yote miwili, na kukumbusha machafuko mabaya yaliyosababisha vifo vya raia wa kigeni mwaka 2008 na 2015.

Matangazo ya kibiashara

Wakazi wanawashutumu wageni, ikiwa ni pamoja na Wanigeria, kuwa chanzo cha biashara ya madawa ya kulevya na ukahaba vilivyokithiri katika vitongoji vyao.

Mwezi uliopita, serikali ya Nigeria ilionyesha hadharani wasiwasi wake baada ya wimbi la mashambulizi shidi ya raia wa kigeni waishio nchini Afrika Kusini.

Jumatatu wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Maite Nkoana-Mashabane, alikutana na mwenzake wa Nigeria, Geoffrey Onyeama mjini Pretoria ili kukabiliana na mvutano huo unaoendelea.

Kila baada ya miezi mitatu, wawakilishi wa nchi mbili hizo, viongozi na wajumbe wa vyama vya kiraia wanakutana kwa ajili ya kushughulikia masuala ya uhamiaji na matatizo ya kuishi pamoja.

Machafuko dhidi ya wahamiaji yamekua yakishuhudiwa kila mara nchini Afrika Kusini, ambapo hali ya maisha nchini humo huvutia mamilioni ya raia wa kigeni, ambao mara nyingi wanatuhumiwa wizi wa kazi za raia wa Afrika Kusini kukuza uhalifu.

Katika mwaka 2015, watu saba waliuawa wakati wa uporaji katika maduka mengi yanayomilikiwa na wageni katika miji ya Johannesburg na Durban. Mwaka 2008 machafuko dhidi ya wageni yalisababisha vifo vya watu 62.