SOMALIA-MAUAJI-USALAMA

Watu wasiopungua watano wauawa katika mlipuko mjini Mogadishu

Askari wa Somalia katika eneo la shambulizi mjini Mogadishu, Januari 2, 2017.
Askari wa Somalia katika eneo la shambulizi mjini Mogadishu, Januari 2, 2017. AFP

Kwa uchache watu watano wameuawa na 10 kujeruhiwa Jumanne hii mchana na mlipuko wa basi la abiria katikati mwa Mogadishu, msemaji wa mji mkuu wa Somalia ameviambia vyombo vya habari.

Matangazo ya kibiashara

Mlipuko huu unatokea siku ambayo Waziri Mkuu mpya wa Somalia Ali Hassan Khaire ametangaza baraza lake la mawaziri.

"Gari lilikua limesimamishwa kwenye kituo cha kukagua magari wakati lililipuka. Kwa uchache watu watano wamepoteza maisha, ikiwa ni pamoja na baadhi ya polisi, na watu kumi kujeruhiwa," amesema Abdifatah Omar Halane.

Maafisa kadhaa waliohojiwa na shirika la habari la AFP wamebaini kwamba ni shambulio la bomu lililotegwa katika gari, ambapo wapiganaji wenye msimamo mkali wa Al Shabab wameongeza katika miezi ya hivi karibuni mjini Mogadishu.

"Mlipuko ulikuwa mkubwa. Nikaona moshi na vumbi katika eneo hilo wakati ambapo nilikuwa juu ya paa la nyumba yangu , " ameeleza mkazi wa eneo la katikati mwa Mogadishu, Yusuf Abdukadir.

Mlipuko ulitokea katika eneo linalopatikana kwenye mita 500 kutoka ofisi ya rais.