SOMALIA

Waziri Mkuu wa Somalia atangaza Baraza lake la Mawaziri

Baadhi ya Mawaziri walioteuliwa na Waziri Mkuu wa Somalia Hassan Ali Kheyre.
Baadhi ya Mawaziri walioteuliwa na Waziri Mkuu wa Somalia Hassan Ali Kheyre. garoweonline.com

Waziri Mkuu wa Somalia Hassan Ali Kheyre amelitaja Baraza lake la Mawaziri katika sherehe iliyofanyika katika mji mkuu wa Mogadishu.

Matangazo ya kibiashara

Baraza hilo lenye Mawaziri 26, kwa mara ya kwanza limewajumuisha wanawake sita ambao watahudumu katika serikali hiyo mpya.

Baraza hili lina mchanganyiko wa Mawaziri wapya na wale waliowahi kuhudumu katika serikali zilizopita.

Kabla ya kuanza kazi, ni lazima majina ya Mawaziri hao yajadiliwe na kupitishwa na Bunge.

Miongoni mwa Mawaziri walioteuliwa ni pamoja na Mwandishi wa zamani na Mhariri wa BBC Idhaa ya Kisomali Yusuf Garaad, ambaye sasa atakuwa Waziri wa Mambo ya nje.

Abdi Farah Juha ameteuliwa kuwa Waziri wa Usalama wa ndani huku Mahdi Ahmed Guled (Khadari), akiteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu.

Wakati hayo yakijiri, serikali nchini humo imetangaza kuwa watu zaidi ya 20 wamepoteza maisha kutoka Kusini mwa nchi hiyo katika jimbo la Jubaland kutokana na baa la njaa.

Wizara ya Mambo ya ndani imesema kuwa vifo hivyo vimetokea ndani ya saa 36 zilizopita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliyezuru Somalia mapema mwezi huu alisema kuwa zaidi ya raia wa nchi hiyo Milioni sita, wanahitaji msaada wa haraka wa chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu ili kuepusha vifo zaidi.