IGAD

Viongozi wa IGAD kukutana Nairobi kujadili hali ya wakimbizi Somalia

Mkutano wa IGAD uliofanyika nchini Somalia mwaka 2016 mjini Mogadishu
Mkutano wa IGAD uliofanyika nchini Somalia mwaka 2016 mjini Mogadishu IGAD

Viongozi wa nchi za muungano wa IGAD kutoka eneo la Afrika Mashariki, watakutana siku ya Ijumaa jijini Nairobi kujadili hali ya wakimbizi wa Somalia waliokimbilia katika mataifa jirani.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huu unatarajiwa kuja na mapendekezo kadhaa na ya muda mrefu kukabiliana na suala hili la wakimbizi ambalo limeendelea kutesa serikali ya Somalia na watu wake.

Hadi sasa raia wa Somalia wapatao Milioni mbili wameyakimbia makwao huku wengi wakiishi nchini Kenya, Ethiopia na nchini Uganda.

Inakadiriwa kuwa wengine zaidi ya Milioni 1 wanaishi nchini humo katika kambi za ndani, katika mazingira magumu.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukitoa wito kwa nchi za IGAD hasa Kenya kuendelea kuwapa hifadhi wakimbizi wa Somalia.

Mahakama nchini Kenya mwezi Februari iliamua kuwa mpango wa serikali kuwarudisha nyumbani maelfu ya wakimbizi wanaoshi katika kambi ya Daadad kwa sababu za kiusalama ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.

Mbali na suala la wakimbizi, baa la njaa ni suala lingine ambalo pia litajadiliwa katika mkutano huo.

Suala la usalama pia litapewa nafasi kubwa katika mkutano huo hasa kuwepo kwa kundi la kigaidi la Al Shabab ambalo limeendelea kuzua hali ya wasiwasi katika eneo la Afrika Mashariki.

Mkutano huu unafanyika baada ya ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteres nchini Somali na kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia nchi hiyo kukabiliana na baa la njaa.