ZIMBABWE

Watu 150 wamepoteza maisha nchini Zimbabwe kutokana na Malaria ndani ya miezi 2

Raia wa Zimbabwe akiwa amebeba mzigo akivuka kwenye moja ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.
Raia wa Zimbabwe akiwa amebeba mzigo akivuka kwenye moja ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko. ZINYANGE AUNTONY / AFP

Watu wanaofikia 150 wamekufa kutokana na ugonjwa wa Malaria nchini Zimbabwe katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, huku watu wanaokadiriwa kufikia elfu 90 wameripotiwa kuambukizwa ugonjwa huu, imesema taarifa ya Serikali ambayo imelaumu mvua kubwa zilizonyesha nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

“Tunashuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa Malaria kwasababu ya mvua zinazoendelea kunyesha mwaka huu na ambazo zimesababisha mazalia ya mbu,” amesema mkurugenzi wa kitengo cha kupambana na Malaria nchini Zimbabwe, Joseph Mberikunashe.

Mberikunashe amesema kuwa wamerekodi vifo vya watu 151 na wengine zaidi ya elfu 90 wameathirika na ugonjwa huu katika kipindi cha miezi miwili, hali iliyosababishwa na mvua pamoja na mafuriko.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa, licha ya kuwa walitarajia kuona kunaongezeka kwa maambukizi ya Malaria kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini humo, lakini wamegundua kuwa vifo vingi vilitokana na wananchi kutopata matibabu ya awali.

“Vifo hivi vingi vimetokana na raia kuchelewa kufika hospitali na wengine kukosa huduma na miundombinu ya afya,” alisema Mberikunashe.

Maeneo yaliyoathirika yanatajwa kuwa ni maeneo ya kusini mwa nchi hiyo ambako kumeshuhudia mafuriko makubwa yaliyosababisha kuharibika kwa miundombinu ya afya.

Mvua kubwa zimeikumba nchi ya Zimbabwe toka mwezi Desemba mwaka jana na Februari mwaka huu, ambapo watu zaidi ya 200 wameripotiwa kufa na wengine zaidi ya 2000 hawana makazi huku shule zikiwa zimeharibiwa vibaya.

Tayari Serikali imeshatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidiwa kukabiliana na hali mbaya ya kibinadamu.