DRC

Maaskofu wa Kanisa Katoliki DRC wasikitishwa na kutotekelezwa kwa mkataba wa kisiasa

Baraza la maaskofu nchini DRC limewasilisha ripoti kuhusu mazungumzo ya kisiasa yaliyofanyika mwaka uliopita na kufikia mkataba wa kuundwa kwa serikali ya mpito kuelekea Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwaka huu.

Maaskofu wa Kanisa Katoliki DRC Kushoto ni Kadinali Laurent Monsengwo Pasinya, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu nchini humo
Maaskofu wa Kanisa Katoliki DRC Kushoto ni Kadinali Laurent Monsengwo Pasinya, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu nchini humo rfi
Matangazo ya kibiashara

Maaskofu hao wameelezea  masikitiko yao kuhusu utekelezwaji wa mkataba huo ambao hadi sasa bado unazua mvutano kati ya serikali na upinzani.

Kifo cha Ettiene Tshisekedi kiongozi wa muungano wa upinzani mwezi Februari, kinaelezwa kuwa sababu kuu inayosababisha pia kucheleweshwa kuanza kwa utekelezwaji kwa mkataba huo.

Viongozi hao wa Kanisa Katoliki wanasema miongoni mwa mambo yanayoleta utata ni vipi Waziri Mkuu atakavyoteuliwa.

Upande wa serikali inayoongozwa na rais Joseph Kabila, inataka upinzani kupendekeza majina matatu lakini upinzani wao wanataka jina moja.

Upinzani umekuwa ukisema, utarejesha mwili wa Tshisekedi nyumbani na kuuzika pale tu serikali ya mpito itakayoundwa chini ya Waziri Mkuu mpya.

Chama cha UDPS sasa kinaongozwa na Felix Tshisekedi, mtoto wa kiongozi wa zamani wa chama hicho na amekuwa akpewa nafasi kubwa ya kuteuliwa katika nafasi hiyo.

Katibu Mkuu wa Baraza hilo Donatien Nshole amesema   raia wa nchi hiyo hawajaridhika na hali ya kisiasa nchini humo na kutotekelezwa kwa mkataba huu na wanasiasa hawajaonesha uzalendo na utashi wa kisiasa.

Hata hivyo, Maaskofu hao hawajasema ikiwa watajiondoa katika usuluhishi wa mgogoro wa kisiasa nchini humo.