GABON

Mazungumzo ya kitaifa yang'oa nanga nchini Gabon

Rais wa Gabon, Ali Bongo Ondimba akizungumza na wanahabari kwenye moja ya mahojiano
Rais wa Gabon, Ali Bongo Ondimba akizungumza na wanahabari kwenye moja ya mahojiano ZACHARIAS ABUBEKER / AFP

Mazungumzo ya kitaifa yaliyoanzishwa na rais wa Gabon, Ali Bongo Ondimba kujaribu kumaliza mzozo wa kisiasa ulioibuka baada ya uchaguzi wa mwezi Agosti mwaka jana na kupingwa na mpinzani wake Jean Ping, yameanza Jumanne ya wiki hii, ripoti ya shirika la habari AFP imesema.

Matangazo ya kibiashara

Sherehe za ufunguzi wa mazungumzo hayo ambayo yanapingwa vikali na Ping pamoja na washirika wake, yalianza majira ya 11 asubuhi kwa saa za Libriville kwenye ikulu ya rais ambapo wanasiasa kadhaa walihutubia mbele wa wajumbe walioalikwa.

Zaidi ya mashirika ya kiraia 1200 pamoja na vyama vya siasa 50 wanashiriki kwenye mazungumzo hayo, ambayo kazi yake ni kutafuta suluhu na ikiwezekana kuongeza muda wa mazungumzo hayo kwa siku 21.

Washiriki wanatakiwa kujikita katika kufanya mabadiliko kwenye taasisi za Serikali, sheria za uchaguzi, kazi za mahakama ya katiba na kutafuta maridhiano ya kitaifa.

Rais Bongo alitangaza kuwa ataitisha mazungumzo ya kitaifa aliyosema yatakuwa huru na wazi, punde tu baada ya kuchaguliwa kwake Septemba 24 mwaka jana.

Matangazo ya kwanza kabisa kuhusu ushindi wake yalizusha vurugu nchini humo katika nchi ambayo inaongozwa na familia ya Bongo kwa miaka zaidi ya 50 sasa.

Mazungumzo haya bado yanapingwa vikali na wanasiasa wa muungano wa Upinzani wa The Coalition for the New Republic CNR unaoongozwa na Jean Ping ambaye bado anasisitiza kuwa yeye ndiye rais aliyechaguliwa kihalali.

Mazungumzo haya yanapaswa kuwa makataa ya awali kuelekea uchaguzi wa wabunge ambao mpaka sas umeahirishwa mara kadhaa mpaka mwezi Julai mwaka huu, lakini unaweza kuahirishwa zaidi ikiwa hakutakuwa na mabadiliko ya katiba na hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu wa karibu na ikulu ya rais Ali Bongo.