NIGERIA-WHO

Nigeria: Homa ya uti wa mgongo tishio watu 270 wameshakufa wengi watoto

Ramani ya shirika la afya duniani WHO inayoonesha eneo la ukanda wa maambukizi ya ugonjwa wa uti wa mgongo
Ramani ya shirika la afya duniani WHO inayoonesha eneo la ukanda wa maambukizi ya ugonjwa wa uti wa mgongo http://gamapserver.who.int/

Watu wanaokadiriwa kufikia 270 wengi kati yao wakiwa ni watoto wamekufa katika kipindi cha miezi mitano iliyopita kutokana na kuugua ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo “Meningitis”, maambukizi yaliyozuka kwenye nchi ya Nigeria, maofisa wa afya nchini humo wamethibitisha.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa wizara ya afya nchini humo mpaka sasa wanao wagonjwa elfu 1 na mia 8 na wamerekodi vifo vya watu 269 kwenye majimbo 15, amesema mkurugenzi wa kitengo cha kupambana na magonjwa ya mlipuko nchini Nigeria, Olubunmi Ojo.

Ojo amesema majimbo matano ya kaskazini mwa nchi hiyo, Sokoto, Zamfara, Katsina, Kebbi na Niger yamekumbwa na maambukizi na kwamba umeanza kuenea kwenye maeneo mengine ya nchi.

Nasir Sani-Gwarzo mkurugenzi wa kitengo cha udhibiti wa magonjwa kutoka wizara ya afya mjini Abuja, amesema miongoni mwa majimbo hayo sita wamerekodi maambukizi kwa watu zaidi ya elfu 1 na vifo 154.

Wizara ya afya nchini humo inasema kwenye mji wa Zamfara peke yake wamerekodi maambukizi kwa watu 590 kati ya watu 29 waliokufa kutokana na ugonjwa huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, vipimo vya kimaabara vinaonesha kuwa ugonjwa huu unaoenea kwa sasa ni aina C.

Shirika la afya duniani WHO, Machi 24 mwaka huu lilisema kuwa watoto wa umri wa kuanzia miaka 5 hadi 14 ndio waathirika wakubwa kwenye maambukizi haya mapya, wakiwa ni nusu ya idadi yote ya watu waliogunduliwa kuwa na maambukizi.

Tayari Serikali inasema imeanza kutoa chanjo maalumu kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo.

Nchi ya Nigeria kwa mujibu wa wataalamu, inatajwa kuwa kwenye ukanda wa mkanda wa maambukizi ya ugonjwa wa uti wa mgongo kusini mwa nchi za jangwa la sahara, ukianzia kutoka Senegal hadi Ethiopia.

Nchi ya Nigeria pamoja na nchi jirani ya Niger zote kwa pamoja zilikumbwa na maambukizi ya ugonjwa huu mwaka 2015 ambapo watu zaidi ya elfu 13 waliambukizwa katika kipindi cha miezi 6 na watu zaidi ya elfu 1 walikufa.

Ugonjwa wa uti wa mgongo unasababishwa na bacteria tofauti, sita kati yao hueneza kwa haraka maambukizi. Ugonjwa huu unaambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kupitia mtu kukohoa au kupiga chafya pamoja na watu kugusana.

Ugonjwa huu husababisha mgonjwa kushindwa kupumua kutokana na sehemu ya ubongo kufunikwa na ute hadi kwenye uti wa mgongo, huku dalili kubwa ikiwa ni kupata homa, kichwa kuuma na shingo kukakamaa.