DRC-UN

Maswali yazuka kuhusu kuuawa kwa watalaam wa Umoja wa Mataifa nchini DRC

Mkoa wa  Kasaï-Oriental, nchini DRC walikotekwa nyara mwezi Machi 2017
Mkoa wa Kasaï-Oriental, nchini DRC walikotekwa nyara mwezi Machi 2017 Wikimedia Commons

Umoja wa Mataifa umethibitisha miili ya watu wawili iliookotwa hivi majuzi ni ya wataalamu wa Umoja huo baada ya kutekwa katika mkoa wa Kasai, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Hali hii imezua maswali mengi kuhusu mauaji haya yaliyolaaniwa vikali.

Swali la kwanza ni kuhusu idadi ya miili iliokotwa. Viongozi wa DRC wanasema waliokota miili ya watu 3 katika kaburi moja, wataalamu hao 2 na mkalimani wao mmoja raia wa nchi hiyo.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa kwa upande wake unasema imekuta miili ya watu wawili pekee ambao ni wataalamu wake, raia wa Marekani na Sweden.

Lakini je, wako wapi raia wengine 3 waliowasafirisha kwa pikipiki ?

Swali lingine lisilokuwa na jibu hadi sasa, ni kina nani waohusika na mauaji hayo ?

Awali msemaji wa serikali ya DRC Lambert Mende alieleza kwamba watalaam hao waliuawa na watu wasiofahamika lakini inaaminiwa kuwa waasi wa Kamwina Nsapu, ndio waliohusika.

Pamoja na hilo, Mende anasema mfumo wa operesheni ya kundi hilo umethibitisha, kwani mtaalam mmoja alikatwa kichwa.

Duru kutoka Kasai hata hivyo zinasema kuwa la Kamwina Nsapu halijawahi kushambulia wageni.

Jambo lingine linazozua utata, ni kwamba mara mbili serikali ya DRC ndio ilikuwa ya kwanza kutoa taarifa ya kifo cha wataalamu hao kabla ya Umoja wa Mataifa wakati ambapo ni wafanyakazi wa Umoja huo.

Maswali yote hayo huenda yakapata majibu baada ya uchunguzi.