DRC

Upinzani nchini DRC waitisha maandamano kushinikiza kutekelezwa kwa mkataba wa kisiasa

Maandamano yaliyopita ya upinzani jijini Kinshasa nchini DRC mwaka 2016
Maandamano yaliyopita ya upinzani jijini Kinshasa nchini DRC mwaka 2016 Wikipedia

Upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeitisha maandamano kote nchini humo siku ya Jumatatu wiki ijayo, lakini pia inawataka  watu kutokwenda kazini ili kumshinikiza rais Joseph Kabila kutekeleza mkataba wa kisiasa uliotiwa saini mwishoni mwa mwaka 2016.

Matangazo ya kibiashara

Muungano huo wa Rassemblement umesema kuwa utahakikisha kuwa shughuli za kila siku katika miji yote nchini humo zinasimama siku hiyo.

Aidha, umeushutumu rais Kabila kwa kushindwa kutekeleza mkataba huo na kuongeza kuwa hali hii imesababisha hali ya usalama kuwa mbya nchini humo hasa baada ya watu kupoteza maisha katika jimbo la Kasai wakiwemo maafisa 39 wa Polisi.

Tangazo hili la upinzani linakuja siku chache baada ya Baraza la Askofu lililoongoza mazungumzo ya kisiasa, kuwasilisha ripoti yake na kusema linasikitika kuona kuwa wanasiasa nchini humo wameshindwa kuutekeleza mkataba huo kwa sababu ya maslahi yao binafsi.

Upinzani na serikali zimeendelea kulaumiana kuhusu utekelezwaji wa mkataba huo.

Suala linaloendelea kuzua mvutano ni uteuzi wa Waziri Mkuu atakayeongoza serikali ya mpito kuelekea Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwaka huu.

Upande wa serikali unataka upinzani upendekeze majina matatu kwa rais Joseph Kabila kumteua Waziri Mkuu lakini upinzani unasema unataka kupendekeza jina moja tu.

Mvutano huu umesababisha kucheleweshwa kwa mazishi ya kiongozi wa upinzani Ettiene Tshisekedi aliyefariki dunia mwezi Februari.

Upinzani umeendelea kusisitiza kuwa Tshisekedi atazikwa tu baada ya Waziri Mkuu kuteuliwa na kuanza kuongoza serikali ya mpito.