Rais Jacob Zuma amfuta kazi waziri wake wa fedha Pravin Gordhan
Imechapishwa:
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amemfuta kazi waziri wake wa fedha Pravin Gordhan baada ya majuma kadhaa ya kuenea kwa uvumi uliotikisa masoko ya nchi hiyo.
Katika taarifa iliyotolewa na ikulu wa Pretoria usiku wa kuamkia leo, imesema kuwa nafasi ya Gordhan sasa itachukuliwa na Mulusi Gigaba.
Mapema juma hili rais Zuma alimuagiza kurejea nyumbani haraka Pravin Grodhan kutoka kwenye ziara yake nchini Uingereza na Marekani.
Kwenye mabadiliko hayo, Sifiso Buthelezi atakuwa naibu waziri wa fedha akiziba nafasi ya Mcebis Jonas.
Kwenye taarifa yake rais Zuma amesema amewaagiza mawaziri wake wapya kufanya kazi usiku na mchana na wafanyakazi wao kuhakikisha wanaleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi ili kutumiza ahadi yake ya maisha bora kwa raia wa Afrika Kusini.
Rais Zuma na Gordhan kwa miezi sasa wamekuwa wakitofautiana kwenye baadhi ya maeneo hali iliyosababisha mgwanyiko hata ndani ya chama cha ANC ambapo kuna maofisa wa juu wanaounga mkono juhudi za Gordhan anayeaminiwa na wawekezaji na mataifa ya magharibi.
Gordhan alikuwa mkosoaji mkubwa wa rais Zuma hasa kuhusua masuala ya rushwa aliyosema imekita mizizi kwenye Serikali yake.