AFRIKA KUSINI

Maelfu waandamana nchini Afrika Kusini kushinikiza kujiuzulu kwa rais Zuma

Mabango ya kumshinikiza rais Jacob Zuma ajiuzulu Aprili 7 2017
Mabango ya kumshinikiza rais Jacob Zuma ajiuzulu Aprili 7 2017 Wikipedia

Maelfu ya raia wa Afrika Kusini wameandama katika miji mbalimbali nchini humo kushinikiza kujiuzulu kwa rais Jacob Zuma.

Matangazo ya kibiashara

Shinikizo hizi zinakuja baada ya rais Zuma, wiki iliyompita kumfuta kazi Waziri wake wa fedha Pravin Gordhan.

Maandamano hayo yamefanyika katika miji ya Pretoria, Johannesburg na Cape Town huku waandamanaji wakisikika wakiimba na kusema wamechoka na uongozi wa Zuma kwa sababu za ufisadi na uongozi mbaya.

Licha ya shinikizo hizi, uongozi wa juu wa chama tawala ANC umemtetea rais Zuma na kusema hakuna haja na ushahidi wa kumlazimisha Zuma kujiuzulu.

Jijini Johannesburg, usalama uliimarishwa huku wafuasi wa rais Zuma wakijitokeza mbele ya chama cha ANC na kuimba nyimbo ya kumsifia kiongozi wao.

Mbali na maandamano haya, wabunge wa chama cha upinzani wamesema kuwa watawasilisha mswada wa kukosa imani na rais Zuma kwa madai ya ufisadi.

Wanaompinga rais Zuma wanasema alimfuta kazi Waziri Gordhan kwa sababu amekuwa katika mstari wa mbele kupambana na ufisadi, huku wanaomuunga mkono wakisema wanaridhika na mabadiliko aliyoyafanya pamoja na uongozi wake.