DRCONGO - SIASA

DRC yakanusha madai ya Umoja wa Ulaya kuhusu utekelezwaji wa mkataba wa kisiasa

Waziri mkuu mpya wa DRC Bruno Tshibala.
Waziri mkuu mpya wa DRC Bruno Tshibala. JUNIOR KANNAH / AFP

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imekanusha kauli ya Umoja Ulaya kuwa uteuzi wa Waziri Mkuu mpya Bruno Tshibala unakwenda kinyume cha  makubaliano ya kisiasa yalioafikiwa mwaka uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Kinshasa imetoa kauli hiyo baada ya kutofanikiwa kwa maandamano ya muungano wa upinzani siku ya Jumatatu kupinga uteuzi huu.

Katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kifaransa ya RFI, msemaji wa muungano wa vyama vinavyomuunga mkono rais Joseph Kabila, Alain Andre Atundu amesema kauli ya Umoja wa Ulaya ni uchochezi kwa raia wa DRC.

Muungano wa upinzani Rassemblement unasema uteuzi wa Bruno Tshibala ni utapeli wa kisiasa nchini humo.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa vyama vya siasa nchini DRC vinastahili kuketi katika meza moja ya moja  na kumaliza tofauti zao ili kumaliza mvutano wa kisiasa unaoendelea.

Muungano wa upinzani umekuwa ukisema kuwa unataka Felix Tshisekedi, kuwa Waziri Mkuu kuongoza serikali ya mpito kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Desemba kwa mujibu wa mkataba huo wa kisiasa.

Ripoti zinasema kuwa baada ya kuitisha maandamano, Tshisekedi aliondoka nchini humo kwenda nchini Ethiopia.