SOMALIA

Watu 28 wapoteza maisha Somaliland kutokana na matumbo ya kuharisha

Mifugo katika eneo la  Somaliland
Mifugo katika eneo la Somaliland N. Williams/Save the Children

Shirika la Kimataifa la Msalaba mwekundu linasema watu 28 wamepoteza maisha katika eneo la Somaliland nchini Somalia kwa muda siku 10 zilizopita baada ya kusumbuliwa na matumbo ya kuharisha.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na vifo hivyo, watu zaidi ya 400 wameathiriwa na wengine 167 kulazwa hospitalini .

Shirika hilo linasema wakaazi wa eneo la Somaliland wanaishi katika mazingira magumu kutokana na baa la njaa ambalo limewafanya watu kula vyakula ambalo vinaonekana kuwa ni hatari.

Inaelezwa kuwa, watu walioathirika zaidi ni wafugaji wanaoishi katika maeneo ya vijijini.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa Somalia ni miongoni mwa mataifa ambayo yanahitaji msaada wa haraka ili kukabiliana na baa la njaa kutokana na ukame unaoshuhudiwa.

Raia wengi wa Somalia hawana chakula na maji safi ya matumizi.

Somaliland ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991, lakini eneo hilo halitambuliwi kama taifa linalojitegemea na Jumuiya ya Kimataifa.