NIGERIA-USHOGA

Watu 53 washtakiwa Nigeria kwa kujihusisha na ushoga

Baadhi ya wanaharakati wa Nigeria wanaotetea ndoa za watu wa jinsia moja
Baadhi ya wanaharakati wa Nigeria wanaotetea ndoa za watu wa jinsia moja Reuters

Waendesha mashtaka kaskazini mwa Nigeria kwenye jimbo la Kaduma wamewashtaki kundi la watu 53 kwa tuhuma za kusherehekea ndoa ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja “Mashoga”.

Matangazo ya kibiashara

Watuhumiwa hawa walikamatwa Jumamosi ya wiki iliyopita, wamekana mashtaka yanayowakabili ambapo mawakili wao wamesema wateja wao wanashikiliwa kinyume cha sheria.

Hata hivyo mahakama imewaachia huru watu hao kwa dhamana ambapo kesi yao imepangwa kusikilizwa tena May 8 mwaka huu.

Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja vimepigwa marufuku nchini Nigeria na adhabu yake ikiwa utapatikana umejihusisha ni kifungo kisichopungua miaka 14 jela.

Wakati wa kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa kwenye mji wa Chediya-Zaria, kundi la watu hao lilikana kujihusisha wala kushiriki kwenye sherehe hiyo na kukana mashtaka dhidi yao.

Wanaharakati wanaotetea ushoga nchini Nigeria wamesema kuwa vijana hao walikamatwa wakati walipohudhuria sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa na sio kwenye harusi kama ambavyo imeripotiwa.

Nchi ya Nigeria inao wakristo wengi wenye msimamo kusini mwa nchi na waislamu wenye msimamo mkali kaskazini mwa nchi hiyo na dini zote mbili zinapinga vikali ndoa za wapenzi wa jinsia moja.

Mwezi January mwaka 2014, The Hisbah au Polisi wa kiislamu kwenye jimbo la Bauchi walivamia maeneo kadhaa na kuwakamata mamia ya watu wakiwatuhumu kufanya vitendo vya Sodoma.

Baadhi ya wanaume hao walipelekwa kwenye mahakama ya sharia kusikiliza shauri lao la kupatiwa dhamana na kundi la watu wenye hasira walishuhudiwa nje ya mahakama hiyo wakishinikiza adhabu kali dhidi yao.

Baadhi ya watu walirusha mawe kulenga mahakama ambayo kesi hiyo ilikuwa ikiendelea hali iliyowalazimu polisi kufyatua risasi hewani kuwatawanya.

Zuio la ndoa za wapenzi wa jinsia moja au usagaji lilianza kutumika mwaka 2014 ambapo kumekuwa na madai kuwa polisi na baadhi ya raia wametumia mwanya wa sheria hiyo kuwanyanyasa watu wanaojihusisha na ushoga ama usagaji, na hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.