DRC-USALAMA

Mapigano ya kikabila yasababisha vifo vya watu 20 Kasai ya Kati nchini DRC

Ramani ya DRC ikionesha jimbo la Kasai ya kati
Ramani ya DRC ikionesha jimbo la Kasai ya kati Wikipedia

Watu 20 wameuawa katika mapigano ya kikabila katika jimbo la Kasai ya Kati nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini humo MUNUSCO limesema mauaji hayo yalifanyika tarehe 19 mwezi huu wa Aprili kati ya makabila ya Lulua-Luba na Chowe-Pende.

Ripoti zinasema kuwa watu wote waliouawa ni kutoka kabila la Chowe-Pende.

Jimbo la Kasai ya Kati limeendelea kushuhudia machafuko tangu mwaka uliopita kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa Kamwina Nsapu.

Wakati uo huo, maafisa wa Umoja wa Mataifa wamezindua mpango wa kukusanya Dola Milioni 65.4 kuwasaidia watu waliokimbia makwao katika jimbo hilo kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu laki 7 wanahitaji misaada ya kibinadamu  kama chakula, makaazi na maji.