Mashirika mbalimbali yalaani hukumu dhidi ya Ahmed Abba

Ahmed Abba, mwandishi wa habari wa RFI katika Idhaa ya Hausa, alihukumiwa Aprili 24 kifungo cha miaka 10 jela na mahakama ya kijeshi ya Yaoundé, nchini Cameroon kwa kosa la  "kutetea na kusaidia ugaidi."
Imehaririwa: 01/05/2017 - 15:31

Hali ya waandishi wa habari inaendelea kuvunjwa katika nchi mbalimbali duniani, hasa nchi nyingi barani Afrika. Wanahabari wanakamatwa, wanafungwa, wananyanyaswa, wanapotezwa hata kuuawa kutokana na kazi yao. Wengin wanatuhumiwa kushirikiana na makundi ya kigaidi, au kutetea makundi ya wahalifu.Hivi karibuni Mahakama ya mjini Yaounde, nchini Cameroon, ilimhukumu mwandishi wa habari wa RFI katika Idhaa ya Hausa Ahmed Abba kifungo cha miaka 10 jela ikimshutumu kutetea na kusaidia ugaidi.Wakati huo huo Shirikisho la Kimataifa la Kutetea Waandishi wa habari (IFJ) limetoa wito kwa wanachama wake kutuma ujumbe wa mshikamano kwa Ahmed Abba.IFJ inasema kwamba mwanahabari huyo hana hatia na amedhulumiwa haki yake, baada ya kukamatwa na kuhukumiwa kutokana na kazi yake.Kesi ya Ahmed Abba iliahirishwa mara 15, baada ya majaji kujenga hoja na tuhuma zisizoeleweka dhidi ya Ahmed Abba.IFJ imeonyesha wasiwasi wake kwamba uhuru wa vyombo vya habari uko hatarini nchini Cameroon kufuatia uamuzi wa mahakam wa kumhukumu Ahmed Abba kifungo cha miaka 10 wakati ambapo hana hatia, na alifanya tu kazi.Ahmed Abba alikamatwa katika mji wa Maroua kaskazini mwa Cameroon Julai 30, 2015. Anatuhumiwa "kula njama katika vitendo vya kigaidi" na "kutotoa taarifa", katika taarifa zake kuhusu mashambulizi ya kundi la Boko Haram.