MAREKANI-SOMALIA

Mwanajeshi wa Marekani auawa Somalia

Nembo ya jeshi la Marekani Africa (Africom)
Nembo ya jeshi la Marekani Africa (Africom) www.africom.mil

Mwanajeshi wa Marekani ameuawa wakati wa operesheni ya kukabiliana na wanamgambo wa Al-Shabab nchini Somalia kifo ambacho kinaelezwa kuwa cha kwanza kutokea katika kipindi cha miaka 24 iliyopita wakati wanajeshi wa Marekani walipokuwa wanashiriki kijeshi nchini Somalia

Matangazo ya kibiashara

Mwanajeshi huyo aliuawa siku ya Alhamisi umbali wa takriban kilomita 64 magharibi mwa mji mkuu Mogadishu, katika mji wa Barii.

Msemaji wa jeshi la Marekani Afrika (Africom) Robyn Mack ameambia AFP kuwa mwanajeshi huyo alipigwa risasi alipokuwa kwenye operesheni ya kushauri na kusaidia Jeshi la Taifa la Somalia na kuongeza kuwa wanajeshi wengine wawili walijeruhiwa katika tukio hilo.

Kuuawa kwa Mmarekani huyo kumetokea siku tatu pekee tangu mkuu mpya wa jopo kazi la Marekani la kuangazia eneo la upembe wa Afrika Brigedia Jenerali David J. Furness kuzuru Mogadishu.