NIGERIA-BUHARI-AFYA

Rais Muhammadu Buhari aelekea London kwa matibabu

Rais wa NIgeria Muhammadu Buhari, ambaye afya yake inaendelea kudorora.
Rais wa NIgeria Muhammadu Buhari, ambaye afya yake inaendelea kudorora.

Mwezi mmoja baada ya kurejea nyumbani akitokea jijini London Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu, rais Nigeria Muhammadu Buhari anarejea tena London kuendelea na matibabu, taarifa ya ikulu ya Nigeria imethibitisha.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa ya madaktari wake inasema kuwa wakifika wataamua atakaa London kwa muda gani wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Taarifa kutoka ikulu ya rais huyo imesema amehitajika kwenda Uingereza kuchunguzwa na madaktari.

Siku ya Jumapili rais Muhammadu Buhari aliwapokea wasichana 82 wa shule ya Chibok, tukio hilo la kuwapokea halikufanywa kuwa sherehe kubwa kutokana na afya yake.

Wanafunzi hao walikuwa wameachiwa huru baada ya kuzuiliwa na wanamgambo wa Boko Haram kwa miaka mitatu.

Wiki iliyopita, rais Buhari hakuhudhuria mikutano mitatu ya baraza la mawaziri huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu hali yake.

Alijitokeza hata hivyo Ijumaa wakati wa swala ya Ijumaa katika msikiti ulio ikulu ya nchi hiyo.
Taarifa kutoka ikulu imesema kiongozi huyo alikuwa amepangiwa kuondoka mapema Jumapili alasiri lakini akachelewa kwa muda kumuwezesha kukutana na wasichana hao wa Chibok.

Rais Buhari amekwenda Uingereza akisema kwamba ana imani kwamba serikali itaendelea kutekeleza vilivyo majukumu yake.