NIGERIA-BUHARI-AFYA

Afya ya rais Buhari imekua ni gumzo Nigeria

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari aendelea kupewa matibabu nchini Uingereza.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari aendelea kupewa matibabu nchini Uingereza.

Raia wa Nigeria wanaendelea kuuliza maswali mengi kuhusu afya ya rais wao Muhammadu Buhari ambaye kwa mara nyingine amekwenda jijini London nchini Uingereza kuonana na madaktari wake.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kurejea nyumbani mwezi Machi akitokea nchini Uingereza alikokaa kwa muda wa miezi miwili, akipata matibabu, ilionekana wazi kuwa angerejea tena nchini humo, hali ambayo imejitokeza tena.

Buhari mwenye umri wa miaka 74, tangu wakati huo hajaonekana katika maeneo ya umma, isipokuwa mwishoni mwa Juma lilipita alipokutana na wasichana wa 82 walioachiliwa huru baada ya kutekwa na magaidi wa Boko Haram miaka mitatu iliyopita.

Wasiwasi wa raia wa nchi hiyo, umeongezeka baada ya msemaji wa rais huyo Femi Adesina kutangaza kuwa haifahamiki ni lini kiongozi huyo atarejea nchini, kwa sababu uamuzi huo upo mikononi mwa Madaktari wake.

Buhari amekabidhi madaraka kwa Makamu wake Yemi Osibanjo huku akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa hana shaka kuwa shughuli za serikali zitaendelea kama kawaida.

Serikali ya rais Buhari imeendela na harakatio za kuimarisha uchumi wa nchi hiyo na kupambana na magaidi wa boko Haram ikiwa ni pamoja na kuendeleza harakati za kuwapata wasicha wa Chibok, lakini jitihada hizi kwa sasa zimeonekana kuzimwa na afya ya kiongozi huyo.