TANZANIA-AFRIKA KUSINI

Jacob Zuma ziarani nchini Tanzania biashara, uchumi kuwa ajenda

Rais wa Afrika kusini, Jacob Zuma ambaye ameanza ziara ya kikazi nchini Tanzania
Rais wa Afrika kusini, Jacob Zuma ambaye ameanza ziara ya kikazi nchini Tanzania REUTERS/Rogan Ward

Nchi ya Afrika Kusini na Tanzania zinatarajiwa kuimarisha uhusiano wao wa kisiasa na kiuchumi katika ngazi ya juu wakati huu ambao rais Jacob Zuma hii leo akitarajiwa kuwa na mazungumzo na mwenyeji wake raia wa Tanzania John Pombe Magufuli kwenye ikulu ya Dar es Salaam.

Matangazo ya kibiashara

Rais Zuma aliwasili jijini Dar es Salaam usiku wa Jumatano kwa ziara ya siku mbili, ambapo marais wote wawili watazungumza na kushuhudia utiaji saini uanzishwaji wa tume maalumu ya pamoja itakayokuwa na jukumu la kutaza uhusiano wa nchi hizo na shughuli za kiuchumi kati ya nchi hizi mbili.

Nchi hizi mbili zina historia ya aina yake toka wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika, ambapo tanzania ilikuwa ni kama nyumbani kwa wapigania uhuru wa taifa hilo ambao waliishi kwenye maeneo ya mkoa wa Morogoro mwaka 1969 ambako ndiko chama cha ANC kilipata uelekeo chini ya rais wa chama hicho wakati huo Oliver Tambo na rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere.

Kwa sasa nchi hizi zinafanya biashara inayofikia randi za Afrika Kusini bilioni 10, Tanzania inatarajia mkutano baina ya marais hawa wawili utachochea kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili kiuchumi na kibiashara.

Rais Zuma hii leo pia atahudhuria kongamano la jukwaa la kibiashara baina ya nchi hizi mbili kongamano ambalo litatumiwa kuainisha fursa za kiuchumi zilizopo baina ya nchi hizi mbili.

Mikataba kadhaa ya ushirikiano pia itashuhudiwa ikitiwa saini.