SOMALIA

Somalia yaomba mataifa yenye nguvu kuisadia kupambana na ugaidi, umasikini na ufisadi

Wajumbe wa Kimataifa waliohudhuria mkutano wa Kimataufa kuhusu Somalia jijini London tarehe 11 mwezi Mei, 2017
Wajumbe wa Kimataifa waliohudhuria mkutano wa Kimataufa kuhusu Somalia jijini London tarehe 11 mwezi Mei, 2017 baahin.net

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed ameyaomba mataifa yenye nguvu duniani, kumsaidia kupambana na ugaidi, ufisadi na umasikini katika nchi yake.

Matangazo ya kibiashara

Mohammed amewaambia wajumbe waliohudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia uliofanyika siku ya Alhamisi  jijini London nchini  Uingereza kuwa maswala hayo ndio yanayoendelea kuisumbua nchi yake kwa muda mrefu sasa, na yanahitaji ufumbuzi.

Viongozi mbalimbali wa dunia na watalaam mbalimbali wamekuwa wakijadiliana namna ya kuisaidia Somalia kuwa taifa thabiti kiuchumi na kiusalama  kufikia mwaka 2020.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteres amesema kuwa taifa hilo linahitaji Dola Bilioni 900 mwaka huu pekee  ili kulisaidia kupambana na ukame ambao umesababisha baa la njaa na kuwaathiri mamilioni ya watu.

Watu zaidi ya Milioni sita wanahitaji msaada wa kibinadamu nchini humo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa ulisema  watoto Milioni 1.4 wanahitaji msaada wa chakula na matibabu kwa sababu wanasumbuliwa na utapia mlo.

Wajumbe katika mkutano huo pia wamejadiliana kuhusu namna Somalia inavyoweza kudhibiti usalama wake wakati jeshi la Umoja wa Afrika AMISOM litapoondoka.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ndiye aliyeongoza mazugumzo hayo hayo yaliyohudhuriwa na marais kutoka mataifa ya Afrika Mashariki ya Kenya, Uganda na Waziri Mkuu wa Ethiopia.