SOMALIA-LONDON

Viongozi wa dunia wanakutana London kujadili namna ya kuisaidia Somalia

Antonio Guterres, katibu mkuu wa umoja wa Mataifa ambaye ataongoza mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia
Antonio Guterres, katibu mkuu wa umoja wa Mataifa ambaye ataongoza mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia REUTERS/Tiksa Negeri

Viongozi wa nchi mbalimbali dunia hii leo wanakutana jijini London Uingereza kutafuta muafaka na nchi ya Somalia mkutano unaolenga kusaidia kudhibiti hali ya usalama nchini humo chini ya utawala mpya.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huu wa siku moja utatazama namna bora ya kupata makubaliano ya pamoja yatakayoshuhudia hali ya usalama inaimarika nchini Somalia na kufikia maendeleo na uchumi imara ifikapo mwaka 2020.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa mkutano huu mjumbe maalumu wa umoja wa Mataifa kwa nchi ya Somalia Michael Keating, ameainisha masuala kadhaa ambayo yatajadiliwa na wakuu wa nchi pamoja na mawaziri kutoka kwenye nchi za ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na mashirika ya kimataifa.

Mkutano huu utaongozwa na wenyeviti wenza rais mpya wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed na katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May.

Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya Federica Mogherini pia anahudhuria mkutano huu sambamba na waziri wa ulinzi wa Marekano James Mattis na naibu waziri wa mambo ya nje Thomas Shannon.

Nchi ya Somalia iko chini ya rais mpya, waziri mkuu mpya na bunge jipya na mkutano huu umejikita katika kupanga mikakati ya kuleta usalama na amani kwenye taifa hilo.

Zaidi ya wajumbe 40 kutoka mataifa mbalimbali duniani, taasisi za kimataifa kama vile benki ya dunia, shirika la fedha IMF na Jumuiya ya nchi za Kiarabu.

Viongozi hawa watajadili namna ya kuinua uchumi wa taifa la Somalia ambalo linaorodheshwa kwenye mataifa ambayo ni masikini zaidi duniani, ambapo pia wakuu hao wa nchi watatafuta namna bora zaidi ya kupata fedha kuisaidia Somalia kwenye utawala.

Deni la zaidi ya bilioni 5 ambalo nchi ya Somalia inadaiwa litaondolewa kwa kutegemea namna ambavyo Serikali mpya itafanya mabadiliko kwenye sekta muhimu za kiuchumi na kupambana na rushwa.