IVORY COAST

Wanajeshi wanaoasi nchini Ivory Coast wawajeruhi watu sita kwa risasi

Wanajeshi wanaoasi nchini Ivory Coast wakiandamana jijini Bouake
Wanajeshi wanaoasi nchini Ivory Coast wakiandamana jijini Bouake REUTERS/Luc Gnago

Wanajeshi wanaoasi nchini Ivory Coast wamewajeruhi watu sita katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Bouake wakati huu wasiwasi ukiendelea kushuhudiwa nchini humo kuhusu hatima ya madai yao.

Matangazo ya kibiashara

Imethibitishwa kuwa waliojeruhiwa  ni wanaume watano na mama mmoja mwenye watoto watatu.

Watu hao wanaendelea kupata matibabu hospitalini mjini Bouake na imeelezwa kuwa walipata majeruhi hayo baada ya risasi zilizokuwa zinafwatuliwa hewani,  kuingia ndani ya makaazi yao.

Ripoti zinasema kuwa watu wengine 15 walipata majeraha madogo na wanaendelea kupata matibabu.

Wanajeshi hao waliomsaidia rais Allasane Outtara kuingia madarakani mwaka 2010, siku ya Ijumaa walianza kuandamana na kuzingira makao makuu ya jeshi jijini Abidjan wakidai ahadi ya malipo yao kutoka kwa serikali.

Fofana, msemaji wa wanajeshi hao 8,400 alijtokeza na kusema kuwa wanajeshi hao wanaomba radhi na wameachana na mpango wao wa kuendelea kushinikiza kulipwa fedha zao.

Waasi hao wa zamani wanadai kulipwa Euro 18,000 kwa kile mwanajeshi, lakini wamefanikiwa kulipwa Euro 7,500 na ripoti zinasema kuwa ilikuwa imepangwa kuwa watapokea malipo mengine mwezi huu.

Hata hivyo, baadhi ya wanajeshi walijitokeza baadaye na kudai kuwa hawakushauriwa kuhusu hatua iliyofikiwa na msemaji wao.

Rais Outtara amekuwa akisema kuwa nchi yake inapitia kipindi kigumu cha kisiasa kwa sababu ya kushuka kwa biashara ya Cocoa.