IVORY COAST

Wanajeshi nchini Ivory Coast waendeleza shinikizo za kulipwa marupurupu yao

Wanajeshi wa Ivory Coast wakiandamana jijini  Bouaké.
Wanajeshi wa Ivory Coast wakiandamana jijini Bouaké. ISSOUF SANOGO / AFP

Milipuko zaidi ya risasi imeendelea kusikika jijini Abidjan na Bouake nchini Cote Dvoire, huku wanajeshi wanaoasi wakiendelea kuandamana na kushinikiza kulipwa marupurupu yao.

Matangazo ya kibiashara

Jijini Abidjan, milipuko ya risasi imesikika katika kambi mbili za kijeshi Mashariki mwa jiji hilo kwa mujibu wa wakaazi wa eneo hilo.

Mji wa pili wa Bouke, milipuko zaidi imeendelea kusikika siku moja baada ya mtu mmoja kupoteza maisha na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa kwa risasi.

Uongozi wa Jeshi nchini humo umetangaza operesheni maalum kuhakikisha kuwa maandamano hayo yanakamilika.

Mkuu wa Majeshi nchini humo Sékou Touré amesema idadi kubwa ya wanajeshi hao wanaoasi wanaokadiriwa kuwa 8,000 wamekubali kuweka silaha chini na kurejea kambini baada ya wito wa rais Outtara.

Inahofiwa kuwa huenda pande hizi mbili zikakabiliana ikiwa mwafaka hautapatikana hivi karibuni.

Waasi hao wa zamani wanadai kulipwa Euro 18,000 kila mmoja lakini hadi sasa wamelipwa Euro 7,500.

Ripoti zinasema kuwa ilikuwa imepangwa kuwa watapokea malipo mengine mwezi huu.

Rais Outtara amekuwa akisema kuwa nchi yake inapitia kipindi kigumu cha kiuchumi kwa sababu ya kushuka kwa biashara ya zao linalotegemewa la Cocoa.