COTE DVOIRE

Wanajeshi walioasi nchini Cote d'Ivoire wakubali kurudi kazini

Maadamano ya wanajeshi wanaogoma mjini  Bouaké Mei 14 2017
Maadamano ya wanajeshi wanaogoma mjini Bouaké Mei 14 2017 ISSOUF SANOGO / AFP

Wanajeshi waliokuwa wanagoma kwa siku nne nchini Cote Dvoire kushinikiza serikali kuwalipa marupurupu  kama walivyoahidiwa mwaka 2010 hatimaye wamekubali kurudi kazini baada ya mwafaka kupatikana.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya serikali kuagiza kuwa wanajeshi hao walipwe marupurupu yao kila mmoja Euro 7,500 na salio linalobaki kulipwa ndani ya miezi miwili ijayo.

Waziri wa Ulinzi nchini humo Alain-Richard Donwahi amethibitisha kuwa serikali imekubaliana na wanajeshi hao ambao tayari wamekubali kurudi kazini na kuondoka mitaani.

Wanajeshi hao ambao zamani walikuwa ni waasi waliomsaidia rais Allasane Outtara kuingia madarakani mwaka 2010, waliahidiwa kulipwa Euro 18,000 kila mmoja kama malipo ya kumsaidia kiongozi huo wa sasa.

Rais Outtara hata hivyo, amekuwa akiwasihi wanajeshi hao kuwa wavumilivu kwa sababu uchumi wa nchi yake unayumba kwa sababu ya kushuka kwa pato la zao la Cocoa.

Wakati wa maandamano hayo, mtu mmoja alipoteza maisha, na zaidi ya wengine 10 kujeruhiwa kutokana na majeraha ya risasi katika katika jiji kuu la Abidjan na mji wa Bouke kulikofanyika maandamano hayo.