DRC-EBOLA

WHO yataja maeneo yaliyoathiriwa na Ebola Kaskazini Mashariki mwa DRC

Ramani ikionesha maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa hatari wa Ebola nchini Tanzania
Ramani ikionesha maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa hatari wa Ebola nchini Tanzania WHO

Maeneo yaliyoathirika na maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yametajwa kuwa Namnwa, Mouma na Ngay.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la afya duniani WHO likishirikiana na Wizara ya afya nchini humo limeripoti kuwa watu wawili wamepoteza maisha katika eneo la Nambwa na wengine 10 kuambukizwa na kuwa eneo lililoathiriwa zaidi.

Eneo la Mouma, mtu mmoja tayari amepoteza maisha huku watatu wakiambukizwa lakini hakuna aliyefariki dunia katika eneo la Ngay ambalo watu sita wameripotiwa kuambukizwa.

WHO inasema kwa ujumla, watu 20 wamethibitishwa kuambukizwa lakini inashukiwa kuwa watu wengine 125 ambao huenda kwa njia moja au nyingine walikuwa katika mawasiliano ya karibu na waathirika wametengwa katika harakati za kuudhibiti ugonjwa huu.

Maeneo yaliyoathirika yapo vijijini na inakuwa vigumu sana kwa watalaam kuwafikia watu waliathirika kwa haraka kutokana na ukosefu wa barabara.

Katika hatua nyingine, Nigeria imesema inachukua tahadhari baada ya ugonjwa huu kuripotiwa nchini DRC.

Mara ya mwisho kwa Ebola kulikumba taifa hilo, ilikuwa ni mwaka 2014 na kusababisha watu 49 kupoteza maisha lakini baadaye maafisa wa afya wakafanikiwa kuudhibiti.

Ugonjwa huu ulisumbua sana Mataifa ya Magharibi mwaka 2013 na kusababisha vifo vya watu 11,300 na kuwambukiza wengine nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia.

Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, kuumwa kwa misuli ya mwili, kuharisha, kutapika, kutokwa kwa damu kutoka maeneo yaliyo wazi ya mwili.

Mtu anaweza kuambukizwa kwa kumshika mnyama aliyeambukizwa, mtu aliyeambukizwa kupitia majimaji ya mwili wake ikiwa ni pamoja na damu.

Watalaam pia wanashauri kuwa mtu aliyefariki duniani kwa sababu ya Ebola asisogelewe wala kuguswa.