DRC-USALAMA

Kiongozi wa kundi la Bundu Dia Kongo atoroka gerezani nchini DRC

Wafuasi wa Ne Muanda Nsemi, waliovamia gereza jijini Kinshasa Mei 17 2017
Wafuasi wa Ne Muanda Nsemi, waliovamia gereza jijini Kinshasa Mei 17 2017 Reuters

Kiongozi wa kundi la kidini linalofahamika kama Bundu Dia Kongo (BDK) akiwa na wafungwa wengine zaidi ya 50, amefanikiwa kutoroka gerezani jijini Kinshasa.

Matangazo ya kibiashara

Serikali jijini Kinshasa imethibitisha kuwa kiongozi huyo Ne Muanda Nsemi, alifanikiwa kutoroka baada ya gereza hilo kuvamiwa na wafuasi wake.

Msemaji wa serikali Lambert Mende amesema  uvamizi huo uliofanyika usiku wa kuamkia leo, na milio ya risasi ilisikika huku kukiripotiwa makabiliano kati ya walinzi wa gereza hilo na wafuasi wa kundi.

Nsemi ambaye anajiita Nabii, alikamatwa mwezi Machi akiwa na wake zake watatu, kwa sababu za uchochezi baada ya wafuasi wake kukabiliana na maafisa wa usalama na kuhatarisha usalama jijini Kinshasa kuanzia mwaka huu.

Kiongozi huyo ambaye pia amekuwa mbunge, amekuwa akisema  anataka kuanzisha upya Ufalme wa Kongo   katika eneo karibu na Mto Congo aliko na ushawishi mkubwa.

Polisi wakishirikiana na jeshi wameanza msako jijini Kinshasa na maeneo mengine kumtafuta kiongozi huyo.