SUDAN-MAREKANI

Marekani yapinga hatua ya Saudi Arabia kumwalika rais Bashir

Rais wa Sudan Omar-al Bashir
Rais wa Sudan Omar-al Bashir Wikipedia

Marekani imesema haiungi mkono hatua ya serikali ya Saudi Arabia kumwalika rais wa Sudan Omar al-Bashir, kushiriki katika mkutano wa nchi za kiarabu na nchi za Kiislamu utakaofanyika siku ya Jumapili.

Matangazo ya kibiashara

Rais Bashir anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya ICC kwa kuchochea na kufadhili mauaji ya zaidi ya watu 300,000 katika jimbo la Darfur.

Ubalozi wa Marekani jijini Khartoum umesisitiza kuwa hauungi mkono mwaliko au kukaribishwa kwa mtu yeyote anayetafutwa na Mahakama ya ICC.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya nje wa Sudan Ibrahim Ghandour amethibitisha kuwa rais Bashir atakwenda katika mkutano huo utakaohudhuriwa pia na rais Donald Trump.

Hii itakuwa ni ziara ya kwanza ya rais Trump nje ya nchi yake baada ya kuingia madarakani mwezi Januari mwaka huu.

Akiwa nchini Saudi Arabia, Trump atawahotubia wajumbe na wakuu wa nchi mbalimbali kuhusu umuhimu wa amani katika nchi za Kiislamu.

Ni ziara inayokuja baada ya rais Trump kuzuia raia kutoka Mataifa saba ya Kiislamu kwenda Marekani, agizo ambalo hata hivyo lilizuiwa na Mahakama.