NIGERIA

Transparency International yasema jeshi la Nigeria limekumbatia ufisadi

Wapiganaji wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria
Wapiganaji wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria REUTERS/Zanah Mustapha

Shirika la Kimataifa la kupambana na ufisadi la Transparency International linasema ufisadi ndani ya jeshi la Nigeria unarudisha nyuma vita dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Matangazo ya kibiashara

Transparency International imesisitiza kuwa hali hii inarudisha nyuma pia juhudi za rais Muhammadu Buhari aliyeingia madarakani mwaka 2015, aliyeahidi kuliangamiza kundi hilo ambalo limesababisha vifo vya maelfu ya watu hasa Kaskazini mwa nchi hiyo.

Shirika hilo linasema kuwa wanajeshi nchini humo wamekuwa wakiingia katika mikataba ya uongo iliyosainiwa nje ya nchini hasa Marekani na Uingereza na kupata idadi kubwa ya fedha.

Mwaka uliopita, serikali nchini humo ilisema kuwa Dola Bilioni 15 ziliibiwa kwa lengo la kununua silaha za kijeshi ambazo hajiziwahi kununuliwa katika vita dhidi ya kundi hili la Boko Haram.

Hata hivyo, madai haya yamekanushwa na jeshi la Nigeria na kusema kuwa madai hayo ya Transparency International si ya kweli.

Meja Jenerali John Enenche, amesema kuwa mengi yamefanywa kuhakikisha kuwa, wanajeshi wanapata mafunzo ya kisasa, kuongeza idadi ya wanajeshi na kununua silaha za kisasa.