DRC-EBOLA

WHO yaonya uwezekano wa maambukizi ya Ebola kusambaa maeneo mengi nchini DRC

Watalaam wa afya nchini DRC wanaopambana na Ebola nchini DRC
Watalaam wa afya nchini DRC wanaopambana na Ebola nchini DRC congovoice.org

Shirika la afya duniani WHO, linaonya kuwa maambukizi ya Ebola Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, yanaweza kusambaa nchi nzima.

Matangazo ya kibiashara

Hadi sasa, watu 20 wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo hatari ambao tayari umesababisha vifo vya watu watatu katika mkoa wa Bas-Uele.

Mapema wiki hii, WHO iliripotiwa kuwa watu 18 ndio waliokuwa wameambukizwa lakini idadi imeongeza na kufikia 20, hali ambayo imeanza kuzua wasiwasi katika eneo hilo.

Mkurugenzi wa WHO anayehusika na maswala ya magonjwa ya dharura Peter Salama amesema kuwa ikiwa ugonjwa huo hautadhibitiwa mapema, huenda ukasambaa nchi nzima na hata eneo la Maziwa Makuu.

Changamoto kubwa ya kuwafikia waathiriwa hao imeelezwa ni miundo mbinu mibaya kama barabara.

Mara ya mwisho kwa Ebola kulikumba taifa hilo, ilikuwa ni mwaka 2014 na kusababisha watu 49 kupoteza maisha lakini baadaye maafisa wa afya wakafanikiwa kuudhibiti.

Ugonjwa huu ulisumbua sana Mataifa ya Magharibi mwaka 2013 na kusababisha vifo vya watu 11,300 na kuwambukiza wengine nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia.

Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, kuumwa kwa misuli ya mwili, kuharisha, kutapika, kutokwa kwa damu kutoka maeneo yaliyo wazi ya mwili.

Mtu anaweza kuambukizwa kwa kumshika mnyama aliyeambukizwa, mtu aliyeambukizwa kupitia majimaji ya mwili wake ikiwa ni pamoja na damu.

Watalaam pia wanashauri kuwa mtu aliyefariki duniani kwa sababu ya Ebola asisogelewe wala kuguswa.