DRC-HAKI

Zaidi ya wafungwa 4,600 watoroka jela ya Makala nchini DRC

Gereza la Makala, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kinshasa (picha ya zamani).
Gereza la Makala, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kinshasa (picha ya zamani). AFP PHOTO / JUNIOR D. KANNAH

Wakazi wengi mjini Kinshasa walilazimika kurudi nyumbani mapema siku ya Jumatano jioni kama ilivyokua kawaida yao kwa siku za nyuma kutokana na hali inayojiri katika mji wa Kinshasa wakati huu, baada ya kutoroka kwa wafungwa wa jela kuu ya Makala.

Matangazo ya kibiashara

Wakazi wa mji wa Kinshasa walichukua tahadhari hiyo ili kuepuka kufananishwa na wahalifu ambao walitoweka baada ya mashambulizi dhidi ya jela kuu ya Makala, ambao polisi imeendelea kuwasaka. Jela hiyo ina uwezo wa kupokea wafungwa 1,500, lakini inaarifiwa kuwa ililikua na wafungwa zaidi ya 7,000.

Kulingana na vyanzo vilivyo karibu na uchunguzi, zaidi ya wafungwa 4600 walitoroka kufuatia shambulio hilo. Ne Mwanda Nsemi (kiongozi wa kiroho wa kundi la Bundu Dia Kongo) na wafuasi wake walikimbia. Kwa mujibu wa polisi, wafungwa wengi hatari na wahusika wa uhalifu mkubwa pia walitoroka.Wito tayari umetolewa ili kuwafichua wahalifu hao ambao huenda wamejificha katika vitongoji vya mji wa Kinshasa, kwa mujibu wa polisi.

Jela ya KRPF, inayojulikana kama jela kuu ya Makala ilijengwa katika enzi za ukoloni, na imekua na tatizo kwa muda mrefu la kupokea wafungwa wengi.

Maafisa kadhaa na mashrika yasiyokua ya kiserikali yalielezea matatizo yanayoikabili serikali kwa kuhudumia maelfu ya wafungwa katika jela hiyo, ambapo wengi wao walikua wakizuiliwa kwa muda. Wafungwa wengine ambao walipewa msamaha wa rais wanaendelea kuzuiliwa katika maeneo machafu.